Tinocco asikilizia ofa

Muktasari:

  • Tinocco alipata nafasi ya kuitwa katika kikosi cha timu  ya Taifa cha Amunike kilichokuwa kinacheza mechi za kufuzu Afcon.

KIPA Benedict Tinocco amejiweka sokoni na kuanza kuangalia maisha ya msimu ujao baada ya kumaliza mkataba wake na Mtibwa Sugar.
Tinocco ambaye aliwahi kuzichezea Kagera Sugar na Yanga, hajui hatma yake ndani ya Mtibwa Sugar aliyoitumikia kwa miaka mitatu kwani hakuna mazungumzo yaliyofanywa juu ya mkataba mpya.
Tinoco amesema kutokana na ukimya wa mabosi wake kunamfanya asijue hatima ya ajira yake ya msimu ujao ndani ya Mtibwa Sugar  hivyo yupo njiapanda hata kwenye maamuzi ya kuanza kusaka timu nyingine .
"Sijajua nitakuwa wapi licha ya kumaliza mkataba wangu na Mtibwa Sugar, hakuna ofa yoyote lakini hilo halinipi presha kwasababu naamini nitakuwa katika ligi msimu ujao," alisema.
Aliongeza licha ya kuwa hana ofa haijamzuia kufanya mazoezi kujiweka fiti kwaajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.
"Naendelea kufanya mazoezi mwenyewe kwasababu kazi yetu hii hakuna kitu kizuri kama mazoezi, lolote linaweza kutokea hivyo lazima mwili uwe na utayari," alisema.
Tinocco alitoka Yanga kwenda kwa mkopo Mtibwa (2016) lakini baada ya kupigwa msasa na kocha wa makipa wa timu hiyo Patrick Mwangata, aliamua kusaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa miaka miwili (2017-2019).