Tino: Nyota Taifa Stars ni wao tu

Muktasari:

  • Wiki hii tena katika mfululizo wa makala hizo tumempata Augustino Peter, maarufu kama Peter Tino, ambaye amefunguka namna alivyohimili changamoto kutoka kwa mashabiki. Ki vipi endelea naye?

WIKI iliyopita katika kuwamulika nyota walioipeleka Tanzania katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 1980, tulianza na kipa Juma Pondamali ‘Mensah’ ambaye alifunguka mambo kibao yaliyowabeba kwenda Nigeria.

Wiki hii tena katika mfululizo wa makala hizo tumempata Augustino Peter, maarufu kama Peter Tino, ambaye amefunguka namna alivyohimili changamoto kutoka kwa mashabiki. Ki vipi endelea naye?

Nyota wengi nchini wamewahi kukumbana na kadhia hiyo ya mashabiki na miaka kadhaa iliyopita, winga Simon Msuva alikutana nayo akiwa kwenye kikosi cha Yanga na mashabiki wa timu hiyo walimzomea.

“Kama huna uvumilivu, hali hii inaweza kumtoa mchezaji kwenye ramani ya mpira,” anasimulia.

ALIVYOPANGUA ZOMEA ZOMEA HIZO

“Unajua tabia za mashabiki wa soka kote duniani kama zinafanana, hawakawii kukugeuka hasa pale wanapoamini unaweza kufunga halafu ukakosa, hawaoni tabu kukuzomea hata kama unachezea timu yao,” anasema.

Anasema enzi zao mambo hayo yalikuwepo sana tu kwa mashabiki waliwazomea kweli kweli, lakini wala hawakujali, hasa yeye, kila walipomzomea ndio kwanza aliongeza ufundi mwingi wa mpira na kuwanyamazisha kiaina. “Sisi zamani, ukizomewa unasema sikubali, unaopambana ili kuwanyamazisha, dakika 90 haziwezi kuisha bila kufanya kitu ambacho mashabiki watake, wasitake utawafunga midomo,” anasema.

SIRI YAKE NI HII TU

Yeyote utakayemuuliza kuhusu Peter Tino atakwambia jamaa alikuwa staa kwenye soka, hata mtaani Kariakoo, Vingunguti na Karume na Tino anafanyia shughuli zake, jina maarufu linalomtambulisha ni staa, halijaja bahati mbaya jamaa anakwambia yeye alikuwa fundi wa soka.

“Acha siku hizi mastaa kwenye soka unawahesabu, zamani sio mimi peke yangu, karibu wote tulikuwa tunajua mpira, sababu ya kujua ilikuwa ni kila mmoja alitaka kuthibitisha anaweza.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga, Pan Africans na Taifa Stars anasema kushindana kwao hakukuwa kwa kuonea wivu na kuchukiana, ilikuwa ni kutaka fulani asikupite, kama akija na mbinu nyingine, mchezaji unafanya juu chini ili umpiku.

ATAMBIA REKODI

Katika maisha yake ya Soka, Tino anakumbukwa kwa namna alivyopachika bao la kusawazisha walipocheza mechi ya marudiano na Zambia (KK 11), bao lililoipeleka Taifa Stars kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 1980.

Anasema nafasi ya Stars kuvunja rekodi hiyo ipo mikononi kwa wachezaji wenyewe kama wataamua iwe hivyo na mtu yoyote kati ya wanaocheza Taifa Stars anaweza kubadili upepo huo mwakani.

NJIA YA afcon

Anasema kufuzu kwao Afcon hakukuanzia uwanjani kulitokana na hamasa waliyokuwa nayo wachezaji kuanzia nje ya uwanja kabla ya mechi hiyo na walitaka kuzima ngebe za Wazambia walioamini Stars watafungwa wakiongozwa na Rais wao uwanjani, Kenneth Kaunda. “Nilimwambia kocha, ninaenda kufunga bao na tunafuzu Afcon, ilikuwa kama vita, hatukukubali kushindwa, tulifikiria namna Watanzania watakavyotupokea, tambo za wapinzani wetu baada ya kushinda, tukahamasishana hakuna kufungwa,” anasimulia.

“Unajua tulipofika Lusaka, timu yetu ilikwenda kumtembelea balozi kabla ya kwenda Ndola. Tukiwa pale (ubalozini) tulionyeshwa magazeti ya Zambia, Rais wao akiwa ameshika funguo za gari na kutamka kwamba kila mchezaji atapewa gari na nyumba kama wataifunga Tanzania,” anasema.

“Yale maneno yalikuwa chachu kwetu, nakumbuka kocha alitueleza ninyi hamjaahidiwa chochote, lakini ninyi ndio mnatakiwa mtoe zawadi kwa Watanzania.

“Kwenye mechi ilikuwa hakuna bahati mbaya. Hadi mapumziko tulikuwa tumeshafungwa bao 1-0. Tukiwa kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kocha alisema wapinzani wetu wanaongoza na bila shaka hawana nguvu, hivyo sisi twendeni tukawafunge.

“Kocha alivyomaliza, peke yangu niliitikia sawa tena kwa sauti ya juu, pale uwanjani kulikuwa na Watanzania kama 30 hivi au 40 waliokuwa wakitushangilia, mashabiki kule walidhani tutakwenda mapumziko tumefungwa mabao matatu au manne.

ILIVYOKUWA

Ilikuwa ni Agosti 26, 1979 jijini Ndola, chini ya Kocha Slowmir Wolk kutoka Poland, akisaidiwa na Joel Bendera na Ray Gama ambao kwa sasa Gama na Bendera ni marehemu.

Ikiwa imepita miaka 11 tangu ianze kushiriki fainali hizo mwaka mwaka 1968, Stars ilihitaji sare ya aina yoyote ili kufuzu Afcon baada ya matokeo ya bao 1-0 jijini Dar es Salaam, Stars iliwafuata Zambia kwao katika mchezo wa mwisho wa lala salama.

Timu hizo zilikuwa zinarudiana baada ya Stars kushinda kwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika wiki mbili zilizotangulia kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam (sasa Uhuru), bao pekee likiwa limefungwa na kiungo, Mohammed Rishard Adolph. Katika mchezo huo wa marudiano, KK walipata bao la mapema katika mchezo huo ambalo lilidumu hadi dakika ya 85.

Dakika tano za mwisho, Peter Tino alisawazisha bao na kunyamazisha umati wa mashabiki waliofurika kwenye Uwanja wa Ndola. Ilipigwa kona kwenda lango la Stars na kipa Pondamali ‘Mensah’ akaupangua kwa ngumi, ukamkuta beki wa kati, Leodegar Tenga ambaye naye alitoa pasi ndefu kwa Hussein Ngulungu. Kiungo huyo akamgongea Tino.

Akiwa amezungukwa na mabeki watatu wa Zambia, Tino aliwazidi ujanja akiwa nje kidogo ya eneo la hatari la Zambia na kupiga kombora la mguu wa kulia, lililompita kipa wa Zambia aliyekuwa kikwazo, John Shileshi.

Katika mchezo huo, Tanzania iliwakilishwa na; Juma Pondamali ‘Mensah’, Leopard ‘Tasso’ Mukebezi, Mohammed Kajole ‘Machela’/ Ahmed Amasha ‘Mathematician’,

Salim Amir, Jella Mtagwa, Leodegar Tenga, Hussein Ngulungu, Omari Hussein ‘Keegan’, Peter Tino, Mohamed Salim na Thuweni Ally.

SAFARI YA SASA

Tino anasema kumfunga Uganda sio jambo gumu kama ambavyo tunadhani wala sio jambo jepesi pia, lakini Watanzania wakiamua The Cranes mbona ‘anakufa’ pale Taifa Machi 22.

“Kwanza ni wachezaji kutulia, kujiamini na saikolojia zao ziwe sawa, waamini mechi ile ni yao na hiyo ndiyo nafasi pekee iliyosalia, kama ilivyokuwa upande wetu mwaka 1979, ingawa sisi tulihitaji sare na wao wanahitaji ushindi.

“Wajitume, kocha afanye kazi yake na Watanzania tuendelee kuwapa moyo tukiamini safari bado ipo, timu yetu ni nzuri, tatizo nadhani tunakosa utulivu na kujiamini,” anasema.