Timu za Bunge Tanzania zaendelea kutamba Burundi

Muktasari:

Michezo ya tisa ya Mabunge ya Afrika Mashariki inayoendelea nchini Burundi inatarajiwa kufikia kikomo kesho Jumapili ambapo timu za Tanzania kwa upande wa soka wanaume Ndugai Boyz watakipiga na wenyeji Burundi. Wanawake netiboli Bunge Queens pia itapambana na wenyeji Burundi.

Timu za Bunge Sports Club za riadha, kuvuta kamba na soka zimeendelea kutamba katika michezo ya tisa ya Mabunge ya Afrika Mashariki inayoendelea nchini Burundi.
Katika mashindano hayo upande wa riadha, Yosepher Komba ameondoka na dhahabu tatu katika mbio za mita mia nne,  mita mia nane na mita 1500.
Katika mbio za Mita mia moja Kenya walitwaa dhahabu wakati Tanzania ilitwa ya fedha kupitia kwa Rose Tweve na Zubeda Sakuru alipata ya shaba.
Rose Tweve kwa mara nyingine aliondoka na fedha katika mbio za mita mia mbili .
Mabingwa watetezi wa kuvuta kamba wanaume walitetea ubingwa wao mbele ya wapinzani wao wote waliokutana nao wakati kwa upande wa soka, Ndugai Boyz wamefufua matumaini ya kuwafuta machozi watanzania baada ya kuwachapa Kenya mabao 2-0, yote yakifungwa na Benjamin Simkanga.
Mashindano hayo yatahitimishwa kesho Jumapili ambapo katika mchezo wa soka Uganda watavaana na Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati Bunge SC maarufu Ndugai Boyz watapepetana na wenyeji Burundi. Netiboli, Bunge Queens itapambana na wenyeji Burundi.