Timu yabebeshwa mabao 9-0 Mombasa

Wednesday April 24 2019

 

By Abdulrahman Sheriff

Mombasa.MASHABIKI wa soka walipata burudani tosha ya kusherehekea sikukuu ya Pasaka kwani walishuhudia jumla ya mabao 73 yaliyofungwa kwenye viwanja mbalimbali za Kaunti za Mombasa, Kwale, Kaloleni na Taita Taveta.

Mabao hayo 73 yalipatikana kutokana na mechi 24 zilizohusisha timu 28, lakini mshangao mkubwa uliwapata mashabiki waliofurika Uwanja wa Dawson Mwanyumba huko Wundanyi ambapo Timu ya Newbies Faraji FC iliibebesha kapu la mabao 9-0 Timu ya Bamba Talent FC.

Katika mechi hiyo ambayo ilihudhuriwa na mashabiki wengi wa nyumbani akiwemo Gavana wa Taita Taveta, Granton Samboja, straika wa Faraji, Emmanuel Mdawida alifunga mabao saba kati ya hayo tisa kwenye dakika za 33, 44, 51, 58, 68, 70 na 83 na kuondoka na mipira miwili.

Ayub Chumo alianza kuona lango la Bamba Talent kutoka Mombasa kwenye dakika ya pili hali bao lingine la Faraji likatingwa nyavuni na Jimstone Mlati katika dakika ya 88.

Kwenye mechi nyingine iliyotoa matokeo ya mabao mengi, Kings United iliishinda Miritini Combined kwa mabao 5-2 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Kwa Shee Primary. Metu Danson alifunga hat-trick hali Dickens Obura akatinga mawili. Wafungaji wa Mikindani walikuwa Salim Chanzera na Fondo Ngao.

Kwengineko, Tsavo Wild Beast iliishinda Haki Afrika 4-3 uwanjani wa Magongo Primary. Duncan Marimba alifunga mabao mawili na Victor Ochieng na Alvin Ngoto wakafunga bao moja kila mmoja kwa Tsavo hali Haki Afrika wakajibia kupitia kwa MacDonald Mtobera mabao mawili Pacific Odhiambo akatinga lingine.

 

 

Advertisement