Timu ya mchezaji Johanna yashushwa daraja Sweden

Wednesday November 8 2017

 

By VINCENT OPIYO

Klabu ya kiungo wa Harambee Stars, Eric Johanna inayotambulika Vasalund IF, imeshushwa daraja nchini Sweden.

Vasalund ilitoka sare ya 1-1 na Umea mechi ya mwisho ya msimu wa daraja la tatu, matokeo yaliyowapeleka nafasi ya tatu kutoka mwishoni mwa jedwali na kujiunga na Enskede na Lulea mkiani watatu hao wakiteremka daraja la nne.

Johanna alipachika bao la kusawazisha kwenye mechi hiyo ya Jumamosi na kufikisha idadi ya magoli yake hadi tano kwenye mechi 21 alizoshirikishwa na timu hiyo aliyojiunga nayo mwakani kutoka Mathare United.

Kwingineko, klabu ya Kolkheti Poti ya ligi kuu ya Georgia hatimaye ilisajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Dila baada ya miezi mitano. Wakenya Amos Nondi na John Macharia walishirikishwa kwenye mechi hiyo ya Jumamosi ugani Poti Park Arena.

Poti ina jumla ya pointi 23 kukiwa kumesalia mechi tatu kutamatisha msimu huu naye beki Abud Omar alicheza mechi yote klabu yake ya Slavia Sofia ikitoka sare ya 1-1 na Botev Plovdiv ligi kuu ya Bulgaria.