Timu ya kikapu yaweka rekodi Kenya

Friday January 17 2020

Timu ya kikapu yaweka rekodi Kenya-Timu ya Taifa ya kikapu-fainali za mataifa ya Afrika-Kombe la Dunia-

 

By Imani Makongoro

Timu ya Taifa ya kikapu imeweka historia ya kufunga pointi nyingi huku ikipanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo wa mashindano ya kutafuta tiketi ya kufuzu fainali za mataifa ya Afrika yanayoendelea nchini Kenya.
Tanzania imeweka historia hiyo jana usiku kwa kuifunga Eritrea pointi 101- 69 huku Ally Mohammed akiibuka mchezaji bora wa mechi hiyo.
"Haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa kwa miaka ya hivi karibuni kushinda pointi zaidi ya 100," alisema Rais wa Shirikisho la Kikapu nchini, Phares Magesa.
Alisema ushindi huo ni mkubwa kwa Tanzania na matokeo ambayo amesema ni kiashiria kizuri katika harakati za msimu huu za kufuzu fainali za Afrika.
Kwa ushindi huo, Tanzania imepanda hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi tatu ikishinda mchezo mmoja na kufungwa mmoja dhidi ya wenyeji Kenya kwa pointi 91-59 siku ya ufunguzi juzi.
Sudan Kusini inaongoza kwenye msimamo ikiwa na pointi nne sawa na Kenya ambayo ni ya pili, lakini zinatofautiana kwa idadi ya vikapu vya kufunga na kufungwa.
Tanzania sasa inahitaji ushindi dhidi ya Sudan Kusini leo jioni na kesho dhidi ya Somalia na Burundi ili kutinga raundi ya pili ya mashindano hayo.
Kocha wa timu hiyo, Alfred Ngalaliji alisema morali ya ushindi leo ni kubwa kwa wachezaji wake ambao, anaamini watafanya vizuri.
"Mchezo wa kwanza tulipoteza sababu ya ugeni na uchovu, ila sina shaka na wachezaji wangu, wamejiandaa na kila mmoja anahitaji ushindi ili tujiweke mahali pazuri kufuzu," alisema.

Advertisement