Timu ya Taifa England ipo hatarini kukosa wachezaji

KAMPENI zimepigwa na wakuu wa soka kwenye Chama cha Soka (FA) cha England pamoja na makocha wa Timu ya Taifa ya England ‘Three Lions’, juu ya haja ya wachezaji wazawa wa England kupewa kipaumbele kwenye klabu za Ligi Kuu ya England (EPL).

 

BY Israel Saria

IN SUMMARY

  • Three Lions wamekuwa wakifanya vibaya, chini ya makocha tofauti, wa ndani na nje ya nchi katika mashindano ya kimataifa, na kufika walau nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka huu nchini Urusi kulichukuliwa kuwa ni mafanikio makubwa kwao.

Advertisement

KAMPENI zimepigwa na wakuu wa soka kwenye Chama cha Soka (FA) cha England pamoja na makocha wa Timu ya Taifa ya England ‘Three Lions’, juu ya haja ya wachezaji wazawa wa England kupewa kipaumbele kwenye klabu za Ligi Kuu ya England (EPL).

Three Lions wamekuwa wakifanya vibaya, chini ya makocha tofauti, wa ndani na nje ya nchi katika mashindano ya kimataifa, na kufika walau nusu fainali ya Kombe la Dunia mwaka huu nchini Urusi kulichukuliwa kuwa ni mafanikio makubwa kwao.

Ilikuwa kawaida yao kuishia hatua za makundi kwenye michuano hiyo au ya Euro, na sababu mbalimbali zimekuwa zikitafutwa ili hatimaye kupata ufumbuzi wa wao kuwa wasindikizaji.

Baada ya kuwa na makocha wa kigeni kwa mara kadhaa, England waliamua kujituliza na kuwa nao wa ndani, akina Roy Hodgson, Sam Allerdyce ‘Big Sam’ ambao hawakupata mafanikio yoyote na sasa Gareth Southgate.

Kabla ya kuanza ligi, Southgate alitoa mwito kwa makocha, hasa wa klabu kubwa 20 zilizo EPL kutoa fursa kwa wachezaji wa England kupata muda wa kucheza zaidi. Kama ni uwekezaji kwenye soka, ni kwamba England ni moja ya nchi zenye miundombinu mizuri zaidi na vifaa kwa ajili ya wanasoka wake, ikilinganishwa na nchi nyingine.

Maandalizi ya timu ya taifa huwa ya kiwango cha juu, lakini inaonekana kwamba tatizo moja kubwa ni wachezaji, na huko tuendako huenda likawa tatizo kubwa zaidi, wote waliocheza Urusi wanatoka England, na wachezaji wengi wa England, kwa muda mrefu sasa, wamekuwa waoga kwenda kucheza nje.

Akademia zimekuwa zikikuza wachezaji vyema, mifano ya Arsenal, Chelsea, Manchester City, Manchester United, na Southampton wanaosifika, lakini baada ya kufuzu inakuwa ngoma kwa chipukizi kukatiza kwenye kikosi cha kwanza, na wakikatiza kupata namba ya kudumu ni ngumu.

Ushahidi unaweza kuonekana kutokana na biashara ya wachezaji inavyofanyika, EPL ikiwa ndiyo ligi maarufu zaidi kote duniani, ikivutia wachezaji wenye vipaji na majina makubwa kutoka pande mbalimbali duniani.

Mamilioni kwa mamilioni ya pauni sasa yanatumika kununua wachezaji na kuwavusha bahari kuja hapa kuchezea klabu, wakikatisha ndoto za chipukizi ambao wanaishia benchi, isipokuwa wachache wanaofanikiwa ‘kutoboa’.

Mfano mmoja ni Jose Mourinho wa Manchester United ambaye kitambo akiwa Chelsea alikuwa shabiki mkubwa wa chipukizi, akiwatumia ipasavyo akina John Terry na wengineo wa England, lakini leo anamkimbia mtu kama Marcus Rashford na kutaka kusajili watu wenye umri wa miaka 30, zaidi au unaokaribia huo kutoka ng’ambo.

Ule utengenezaji vipaji na kuwapandisha wachezaji taratibu unakufa, makocha wakitaka kubishana kwa kusajili kwa fedha kubwa kutoka nje. Tazama Manchester City wa Pep Guardiola lakini pia Arsenal wamebadilika kabisa kisera tangu miaka ya mwisho ya Arsene Wenger, wakinunua watu kutoka Ufaransa, Hispania, Ujerumani na kwingineko huku majina makubwa ya wachezaji wao chipukizi wa England wakiwa hawana la kufanya zaidi ya kwenda ama kwa mkopo klabu ndogo au kuuzwa kabisa. Ndiposa wakaondoka akina Kierran Gibbs, Theo Walcott, Carl Jenkinson na wengineo kutafuta maisha.

Ajabu ni kwamba, katika kipindi cha miezi 15 iliyopita, timu za vijana za taifa la England, anzia chini ya miaka 17 hadi chini ya miaka 21 wamekuwa wazuri na kutamba duniani, katika makombe ya dunia na Ulaya, ikionekana kwamba ni matunda mazuri kwa wakati ujao kirahisi.

Hata hivyo, ukienda kwenye kituo na ofisi za soka pale St George’s Park, kuna kila sababu ya kuwa na hofu kwamba mafanikio yaliyopatikana walau kidogo mwaka huu yanaweza yasiwe endelevu.

Hii inatokana na ukweli kwamba takwimu zinaonesha kwamba idadi ya wachezaji wa England waliopata fursa ya kucheza kwenye mechi nne za kwanza za EPL msimu huu ni asilimia 30.4 tu, yaani ikishuka kutoka asilimia 33 ya msimu wa 2017/18.

Kama nilivyotangulia kusema, ni kwamba makocha wanapigana vikumbo kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi, na wakiisha kutumia kiasi kikubwa cha fedha, hawatarajiwi kuwaweka benchi nyota hao, bali watakaoyasugua ni chipukizi hawa wa England.

Asilimia ya wachezaji waliopata fursa ya kucheza kwenye klabu zile sita kubwa – Arsenal, Chelsea, Liverpool, Manchester City, Manchester United na Tottenham Hotspur ni karibu 20 tu. Ni mbaya kwa England, kwa sababu hizi ni klabu ambazo zingewatumia wachezaji wazawa na kuwaingiza kwenye soka ya Ulaya – Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na Ligi ya Europa. Sasa hawachaguliwi, ngumu kucheza huko na kukua uzoefu wao.

Yapo mambo mengi chanya yanaonekana kwa England, lakini tatizo linakuja hapo kwenye muda wa kucheza soka, zile dakika muhimu kwa hawa wa England kusakata soka, kutokana na nguvu ya fedha kwenye soka na aina ya makocha na wamiliki wa klabu waliopo England, ambapo klabu zinauzwa kila uchao na mtu mmoja mgeni anakuwa na sauti na kuleta wachezaji anaotaka. Ujerumani wamejiweka vyema; wakizuia umiliki wa mtu mmoja, hivyo kwamba watu wa eneo fulani wanaimiliki klabu yao, na hao watawatumia sana wachezaji wao, ndiyo maana tunaona majina ya wachezaji wa klabu za Bundesliga mengi ni Wajerumani.

Ikiwa wadogo hawa wanatiwa moyo kuingia kwenye akademia za klabu, wakipanda na kuwa bora duniani kwenye timu ya taifa U-17 hadi U-23, kimantiki ingetarajiwa watoboe bila shida kwenye vikosi vya kwanza vya klabu za EPL, maana tangu kuanza msimu huu wa soka, ni wachezaji 17 tu wenye umri chini ya miaka 21 wamecheza EPL, hiyo ni ndogo zaidi ya wachezaji wa nyumbani katika ligi tano kubwa duniani – England, Hispania, Italia, Ufaransa na Ujerumani. Huko kwingine wanajali zaidi wa nyumbani.

More From Mwanaspoti
This page might use cookies if your analytics vendor requires them. Accept