Timu ya Raga, ‘Shujaa 7s’ yapata kocha mpya

Saturday October 6 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Hatimaye kitendawili cha nani atarithi kiatu cha kocha wa sasa wa timu ya taifa ya mchezo wa Raga ya Kenya, ‘Shujaa 7s’, Innocent Simiyu ‘Namcos’, kimeteguliwa baada ya Kocha wa Homeboyz RFC, Paul ‘Pau’ Murunga kukabidhiwa mikoba hiyo.

Uamuzi wa kumteua Murunga aliyeiongoza Homeboyz kutwaa ubingwa wa taifa, umefikiwa na shirikisho la mchezo huo nchini (KRU), baada ya kufanya mchujo wa mwisho kwenye usaili, uliohusisha wakufunzi 12, ambao walikuwa wanawania nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana ilisema Murunga atachukua mikoba hiyo rasmi baada ya kumalizika kwa mashindano ya ubingwa wa Afrika, ambayo yataongozwa na Namcos, yakiwa ni majukumu yake ya mwisho.

Murunga anatarajiwa kuchukua usukani katika msimu mpya wa misururu ya ubingwa wa Dunia, maarufu kama, ‘2018/19 HSBC World Sevens Series’, na atasaidiwa na Kocha mkuu wa timu ya wanawake ‘Kenya Lioness’ na Mwamba RFC, Kevin Wambua.

Aidha, kwa mujibu wa mabadiliko hayo, Kocha wa ukakamavu, Geoffrey Kimani na mwenzake wa viungo Lameck Bogonko, watasalia katika majukumu yao ambapo Oktoba 13, mwaka huu, watashirikiana na Simiyu kuiongoza Shujaa 7s katika mashindano ya ubingwa wa Afrika.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa KRU, Sylvia Kamau ni kuwa, Uongozi mpya wa Shujaa 7s, utasaini mkataba wa miaka miwili. Hii ni mara ya pili kwa Murung kuitumikia timu ya taifa, kwani aliwahi kuwa msaidizi wa Kocha wa zamani, Benjamin Ayimba (msimu wa 2015/16), ambaye ni mtangulizi wa Innocent Simiyu.

Kutokana na uzoefu wa kufanya kazi chini ya Ayimba na kupata mafanikio makubwa, ambayo ni pamoja na kushinda msururu wa Singapore 7s pamoja na kuisaidia Shujaa kufuzu michuano ya Olimpiki ya mwaka 2016.

Jumla ya makocha 12 walijitokeza katika mbio za kuwania nafasi ya kurithi mikoba ya Simiyu, saba kati yao wakiwa ni makocha wa kigeni huku watano wakiwa ni wazawa. Baadhi ya wakufunzi wa kigeni waliojitokeza ni pamoja na Liam Middleton (Zimbambwe), Nick Wackley (Wales), Richie Williams (Wales), na Malik Chachibara (Fiji).