Timu nne zaweka rekodi tofauti RBA

Wednesday July 29 2020

By Imani Makongoro

WAKATI Ligi ya Mpira wa Kikapu mkoa wa Dar es Salaam (RBA), ikiendelea usiku wa leo Jumatano kwa mechi kati ya Savio na Vijana, timu nne zimeweka rekodi tofauti mpaka sasa.

JKT na Pazi ndizo timu pekee zenye rekodi ya kutofungwa mpaka sasa kwenye ligi hiyo inayoendelea Uwanja wa Bandari, Kurasini.

Hata hivyo, Don Bosco Youngstars na Magnets nazo zimeweka rekodi ya kutoshinda mchezo wowote mpaka sasa kwenye ligi hiyo ambayo kila timu imebakisha mechi tisa kumaliza msimu.

Youngstars ni ya pili kutoka mwisho katika msimamo ikiwa na pointi 6 baada ya kucheza mechi sita na kufungwa zote wakati Magnets ni ya mwisho ikiwa na pointi tano baada ya kufungwa mechi zote tano ilizocheza.

JKT ndiye kinara katika msimamo ikiwa haijafungwa mechi zote sita alizocheza na kuvuna pointi 12 sawa na Pazi ambaye ni ya tano na imecheza mechi tano ikiwa na pointi 10 na mechi moja zaidi mkononi.

Timu ya jeshi ya ABC ni ya pili ikiwa na pointi 11 baada ya kushinda mechi tano na kufungwa moja, sawa na Kurasini Heat ambayo ni ya tatu, timu hizo zikitofautiana kwa idadi ya pointi za kufunga na kufungwa.

Advertisement

Vigogo Savio ni wa nane wakiwa wamecheza mechi tano na kushinda tatu, mechi sawa na za Oilers ambayo ni ya 11 katika msimamo baada ya kufungwa mechi tatu kati ya tano walizocheza.

Advertisement