Timu Ligi Kuu zashtukia ukuta Yanga, Simba unapitika!

Muktasari:

Swali kubwa katika mijadala ya wapenda soka lilikuwa, nani atakuwa wa kwanza kuifunga Yanga.

HATIMAYE bao la dakika ya 89 kutoka kwa ‘mfia timu’, Jacob Massawe wa Stand United dhidi ya Yanga, limeleta msisimko mpya kwenye msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Yanga, ambao wanaongoza ligi, walikuwa na kasi isiyo ya kawaida kuelekea kuusaka ubingwa wa 28 wa Tanzania Bara.

Swali kubwa katika mijadala ya wapenda soka lilikuwa, nani atakuwa wa kwanza kuifunga Yanga.

Kucheza mechi 19 na kushinda 17 na sare 2 pekee, haikuwahi kutokea Tanzania tangu kuanza kwa ligi ya kitaifa, mwaka 1965.

Hata ile misimu ambayo Simba na Azam FC walikuwa mabingwa bila kupoteza hata mchezo mmoja, hawakuwa na matokeo kama haya.

Kwa hiyo mwamba mwenye kuweza kuisimamisha timu yenye kasi kama hii, inapaswa kutajwa angalau kwa wiki moja, kama sio hadi itokee timu nyingine ndogo ifanye maajabu.

Lakini bahati mbaya ni kwamba ushindi wao ulifunikwa na matokeo ya Simba dhidi ya AS Vita.

Sasa kupitia ukurasa huu, tunajaribu kuliweka juu kidogo katika mahali linapostahili kuwepo jina la miamba hawa wa Shinyanga, nchi ya Igembe Nsabo.

NI UNITED

Hii ni timu inayotokea Shinyanga mjini katika kituo kikuu cha zamani cha mabasi ya mikoani. Wapiga debe na wafanyabiashara wengine wa sokoni pale wakaungana na kuanzisha timu waliyoiita Stand United yaani Muungano wa Stendi.

Muungano kwenye mpira sio jambo geni hapa nchini lakini hapo kabla hakukuwa na utamaduni wa kutumia jina la United kuuenzi Muungano huo hadi miaka ya 1990 pale watanzania walipoanza kufuatilia mpira wa nje.

Zikazuka timu kama Moro United, Singida United na hatimaye ndiyo hawa Singida United.

Muungano unaozungumziwa hapo unaweza ukawa wa timu zaidi ya moja au watu wa aina tofauti wanapokuja pamoja.

Kupitia Stand United, Mzee wa Upupu anakufungua kifikra kwa kukupa asili ya klabu nyingine duniani vinavyotumia jina la UNITED.

WAKINA UNITED WENGINE

Kila nchi huwa na utamaduni wa majina ya mazoea yatakayoambatana na majina rasmi kwa klabu zake na kila watu wana historia yao inayobeba maana halisi ya maneno yanayotumika.

Kwa mfano, asilimia kubwa ya klabu za Hispania hutumia neno la REAL; kama Real Madrid, Real Betis au Real Sociedad.

Uturuki hutumia neno Spor; kama Alanyaspor, Antalyaspor, Trabzonspor, Kayserispor, Bursaspor nk.

Kwa hawa wakina United, asili yao ni England ambako utakutana na Manchester United, Newcastle United, Leeds United, West Ham United na hadi ligi za chini kabisa kwenye timu kama Thame United, Wrexham United nk.

Timu ya kwanza kutumia jina la United ni Newcastle pale timu mbili za Newcastle East End (ambayo mwanzo kabisa iliitwa Stanley FC) ilipoungana, kwanza na Rosewood FC, halafu ikachukua baadhi ya watu kutoka timu iliyokufa ya Newcastle West End na kuzaliwa Newcastle United mwaka 1892.

Baada ya hapo, zikazaliwa United nyingine nyingi. Juu kabisa, nilizungumzia kuhusu UNITED kutokana pia na Muungano wa watu wa aina tofauti, zaidi ya kuungana timu.

England kama moja ya mataifa makubwa na yenye uchumi bora duniani, huvutia watu kutoka kila pande ya dunia.

Watu hawa ndio wakati mwingine huweka kando tofauti zao na kuungana kuunda timu moja.

Hapa ndipo utaipata klabu kama West Ham United ambapo wafanyakazi wa kiwanda cha chuma cha Thames Iron Works waliokuwa na asili ya nchi mbalimbali duniani, walipoamua kuunda timu yao na mwaka 1900, timu hiyo ikiwa na miaka mitano, wakaamua kuiita West Ham United.

Hawa wanaoitwa Mashetani Wekundu, Manchester United, hapo kabla walikuwa wakiitwa Newton Heath na mwaka 1902 ndipo wakajibadilisha na kujiita Manchester United.

Na hii ni baada ya matajiri wanne, akiwemo mchezaji wao Harry Stafford na mtengeneza bia, John Henry Davies, kuunganisha mitaji yao na kuinunua klabu hiyo iliyokumbwa na ukata kiasi cha kukaribia kufilisika.

Katika wote hao, mkasa wa Leeds United ni wa kipekee. Hawa walianza kama Leeds City mwaka 1904 lakini mwaka 1919 wakakumbwa na kashfa kubwa ya malipo yasiyo halali kwa wachezaji wao.

Hii ilikuwa kashfa kubwa iliyochafua jina lao na katika kujisafisha, wakaamua kuondoa City na kuweka United...hawakuwa na sababu yoyote ya kimuungano.

Haya tusingeyajua kama sio Stand United kutufungulia milango ya mbio za ubingwa iliyoonekana kujifunga huku Yanga wakikaribia kuingiza mguu mmoja.

Lakini pia ahsanteni Yanga kwa kutuonesha kwamba licha ya fedha kuwa kitu muhimu sana katika kuendesha mpira, maisha yanaweza yakaendelea pale inapokosekana. Mliionesha nchi kuwa mnaweza kushinda, sasa ilikuwa zamu ya kuionesha kuwa mnaweza kushindwa.