Timo Werner aifuta Chelsea kwenye ubingwa msimu huu,hatubebi

LONDON, ENGLAND. Hatuwezi kubeba. Hicho ndicho unachoweza kueleza kuhusu kauli ya straika mpya wa Chelsea, Timo Werner aliyedai The Blues hawawezi kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu licha ya kutumia Pauni 210 milioni kunasa mastaa wapya.

Straika Werner alitua Chelsea akinaswa kutoka RB Leipzig kwa ada ya Pauni 48 milioni, huku mastaa wengine walionaswa kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi ni Kai Havertz - aliyenaswa kwa Pauni 70 milioni, Ben Chilwell kwa Pauni 50 milioni na Hakim Ziyech kwa mkwanja wa Pauni 36 milioni.

Kocha wa The Blues, Frank Lampard alimnasa pia beki wa kati Thiago Silva kwa uhamisho wa bure kutoka Paris Saint-Germain, lakini akilipwa mshahara mkubwa.

Lampard anakaribia pia kukamilisha uhamisho wa kipa Eduardo Mendy kutoka Rennes kwa ada ya Pauni 25 milioni huku kikosi chake kikiendelea kuhusishwa na mpango wa kumsajili kiungo wa West Ham United, Declan Rice kwa ada ya Pauni 45 milioni.

Werner, ambaye alifunga mabao 36 kwenye Bundesliga msimu uliopita akiwa na kikosi cha RB Leipzig, anadhani Chelsea mpango wake haoni kama utakuwa tayari na kuchuana kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Maneno hayo yanaweza yasimfurahishe mmiliki bilionea Roman Abramovich, ambaye amewekeza pesa nyingi kwenye kikosi hicho ili kuhakikisha timu inabeba mataji na kurudisha ubabe Stamford Bridge. Werner, 24, aliliambia gazeti la Bild: “Lazima tuwe wakweli na kwa kusema hilo hatuwezi kushinda Ligi Kuu England wala Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

“Kama itafanikiwa, basi litakuwa jambo zuri. Lakini, hilo si ambacho klabu inatarajia. Nataka kuwalinganisha na Liverpool kwa miaka michache iliyopita. Katika mwaka wao wa kwanza hawakubeba ubingwa. Mwaka wa pili walifika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, mwaka wa tatu walishinda taji la Ulaya na mwaka wa nne, walibeba Ligi Kuu England.

“Kulingana na mipango yetu Chelsea, tunataka kuboresha mambo hatua kwa hatua kufikia malengo ya kubeba ubingwa katika kila msimu.” Kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp alimhitaji straika huyo Mjerumani, lakini mabosi wake wa huko Anfield hawakuwa tayari kulipa Pauni 48 milioni.

Werner alisema: “Nilihitaji kufanya uamuzi sahihi mimi binafsi. Kwenye kikosi cha Chelsea, niliona kabisa kwamba nakwenda kupata nafasi ya kucheza moja kwa moja. Kwa mipango iliyopo, naweza kukuza soka langu.

“Hii ni nafasi ambayo Sadio Mane au Mohamed Salah waliizingatia miaka minne au mitatu iliyopita walipotua Liverpool. Walihitaji kwenda hapo kukuza vipaji vyao na hatimaye wameshinda Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya.”

Werner alishuhudia kikosi chake cha The Blues kikichapwa 2-0 na Liverpool kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa uwanjani Stamford Bridge juzi Jumapili, ambapo Mane alifunga mabao yote mawili.