Thiago Alcantara awekea bifu VAR

Muktasari:

Thiago, ambaye alianza katika kikosi cha Bayern pamoja na Javi Martinez katika kiungo, amesema tangu kuanzishwa kwa VAR watu wanashindwa kushangilia vyema magoli.

MUNICH, UJERUMANI. HII vita aliyoianzisha Thiago Alcantara ni kama kupigana na ukuta.
Kiungo huyo wa Bayern Munich, ameiwekea bifu teknolojia ya VAR akisema haipendi kinoma maana inaua hisia ya mchezo wa soka.
Kufuatia timu yake ya Bayern kupigwa 2-1 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Arsenal juzi Alhamisi, kiungo huyo raia wa Hispania mwenye asili ya Brazil, amejia juu matumizi hayo ya teknolojia hiyo katika kumsaidia muamuzi.
"Sikubaliani kabisa na VAR," alisema. "Nina mahaba na soka na napenda utata unaotokea mchezoni. Bila ya utata, tusingekuwa na matukio ya kihistoria ya soka.
"Teknolojia zinasaidia kuleta haki kiasi, lakini zinaua hisia za mchezo," alisema nyota huyo wa zamani wa Barcelona.
Thiago, ambaye alianza katika kikosi cha Bayern pamoja na Javi Martinez katika kiungo, amesema tangu kuanzishwa kwa VAR watu wanashindwa kushangilia vyema magoli.
"Unapoenda kushangilia, unaenda huku ukiwa na shaka tele.
"Unamuangalia refa kujua kama ni goli au ameweka mkono sikioni mwake (kuashiria anataka liangaliwe kwenye kwenye VAR).
"Naamini hili linaufanya mchezo wa soka kupoteza hisia," alisema.