The Big boss, Cavani kulipwa kibosi Man Utd

MANCHESTER, ENGLAND. STAA, Edinson Cavani anajiandaa kuwa mmoja wa wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa Manchester United.

Straika huyo wa Uruguay, ambaye ni mchezaji huru jana alikuwa kwenye hatua za mwisho kukamilisha uhamisho wa kutua Old Trafford. Man United iliweka mkazo kunasa huduma ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Napoli na Paris Saint-Germain baada ya kusuasua kumnasa mchezaji iliyekuwa inamsaka kwa nguvu zote, Jadon Sancho.

Dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi lilitarajia kufungwa jana Jumatatu na baada ya kichapo cha mabao 6-1 kutoka kwa Tottenham Hotspur kwenye mchezo wa Ligi Kuu England, Man United inahaha kuweka mambo sawa kuboresha kikosi baada ya kusajili mchezaji mmoja tu kabla ya kufikia siku ya jana.

Cavani aliachana na PSG mwishoni mwa msimu uliopita baada ya mkataba wake kumalizika, hivyo atatua Old Trafford bure. Hata hivyo, haina maana kwamba atapatikana kwa pesa kiduchu. Kinachoelezwa ni kwamba Cavani atalipwa mshahara wa Pauni 200,000 kwa wiki sawa na Pauni 10.4 milioni kwa mwaka. Makamu mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward amemwandalia Cavani mkataba wa miaka miwili - ambao utamfanya avune Pauni 20.8 milioni kwa muda huo.

Wakati Cavani akitarajia kuvuta mkwanja huo mrefu, mshahara wake atakuwa amezidiwa na wachezaji watatu tu kwenye kikosi hicho cha Man United.

Kipa David De Gea - ambaye juzi Jumapili aliokota mipira mara sita kwenye mchezo wa Spurs, ndiye anayelipwa mkwanja mrefu zaidi, Pauni 375,000 kwa wiki.

Kiungo Paul Pogba, anafuatia kwa kulipwa Pauni 290,000 kwa wiki na kwenye namba tatu yupo Anthony Martial anayelipwa Pauni 250,000 kwa wiki - ikiwa hao ni wachezaji watatu wanaolipwa mzigo mkubwa kuliko Cavani.

Cavani ambaye hajacheza mechi yoyote tangu Machi huku mara yake ya mwisho kufunga bao ilikuwa Februari, kwa mshahara atakaolipwa huko Old Trafford atalingana na Marcus Rashford.

Mabosi wa Man United wanaamini kwamba usajili wa Cavani unaweza kuwa sawa na ule wa Zlatan Ibrahimovic ambao ulikuwa na mafanikio makubwa.

Ibrahimovic alifunga mabao 29 katika msimu mmoja tu huko Man United aliponaswa akiwa na umri wa miaka 35. Pia Man United wanaamini ujio wa Cavani utawasaidia kuwapa uzoefu washambuliaji vijana kwenye kikosi hicho.

Anatua Man United akiwa na takwimu kibao zenye kufurahisha kwa mashabiki wa Old Trafford. Kwenye mechi 138 alizochezea Napoli kuanzia 2010 hadi 2013 alifunga mabao 104. Baada ya hapo alikwenda PSG na kucheza kwa miaka saba, ambapo alifunga mabao 200 katika mechi 301 na kuwa kinara wa mabao wa muda wote kwenye kikosi hicho cha matajiri wa Ufaransa.

Man United inaomba staa huyo aendeleze makali yake kwenye kutupia nyavuni hasa baada ya kutua kwenye kikosi chao ili kuendana na malipo ya mshahara mkubwa wanaomlipa.