Tetemo la mshahara

Muktasari:

  • Sanchez mwenyewe hayupo tayari kushusha mshahara wake ili kuondoka kwenye timu hiyo. Hata hivyo, Sanchez si mchezaji pekee wanaozipasua kichwa timu zao kwa maana ya kushindwa kuwauza hata kama haiwataki kwenye vikosi vyao.

LONDON, ENGLAND.MAISHA ndivyo yalivyo. Wahenga walisema hivi, mtoto akichezea moto mwaache umuunguze. Hicho ndicho kinachowakuta klabu vigogo wa huko Ulaya kutokana na dili walizowapa mastaa wao ambao kwa sasa itakuwa shida kubwa kuwapiga bei hata kama haiwahitaji kwenye vikosi vyao.

Alexis Sanchez amekuwa shida kubwa huko kwenye kikosi cha Manchester United ambapo mshahara wake anaolipwa mkubwa umedaiwa kuibua matatizo makubwa ndani ya kikosi hicho. Kila staa kwa sasa anataka kulipwa mshahara mkubwa kama anaolipwa staa huyo, huku mabosi wa timu hiyo wakipata shida kutafuta mteja wa kumpiga bei kwa sababu mchezaji mwenyewe hauziki.

Ugumu unakuja sehemu moja tu, hakuna timu nyingine itakayokuwa tayari kulipa mshahara mkubwa kama anaolipwa huko Old Trafford. Man United inamlipa mshahara wa Pauni 350,000 kwa wiki staa huyo wa kimataifa wa Chile. Hakuna timu nyingine iliyotayari kumlipa Sanchez mshahara kama huo na jambo hilo linawafanya Man United kuendelea kubaki na mchezaji huyo kwenye kikosi chao hadi mwisho wa mkataba wake.

Sanchez mwenyewe hayupo tayari kushusha mshahara wake ili kuondoka kwenye timu hiyo. Hata hivyo, Sanchez si mchezaji pekee wanaozipasua kichwa timu zao kwa maana ya kushindwa kuwauza hata kama haiwataki kwenye vikosi vyao.

Gareth Bale ni shida huko Real Madrid, ambapo staa huyo hauziki kwa sababu ya mshahara wake anaolipwa huko Bernabeu. Hakuna timu iliyokuwa tayari kumlipa staa huyo mshahara mkubwa kama anaolipwa na Los Blancos. Bale anapokea Pauni 350,000 kwa wiki. Mesut Ozil wa Arsenal naye anaingia kwenye orodha hiyo.

Bila shaka wababe hao wa Emirates watahitaji sana kuachana na mchezaji huyo wanayemlipa Pauni 300,000 kwa wiki, lakini shida ni kwamba hakuna timu yenye uwezo wa kumchukua mchezaji huyo kwa kiwango chake cha sasa na kumlipa mshahara kama anaopewa na Arsenal.

Mchezaji mwenyewe hataki kushusha mshahara wake na ndio maana inakuwa shida na kuendelea kubaki kwenye timu zao wanazocheza pengine hadi mwisho wa mikataba yao.

Paul Pogba wa Man United linaweza kumkumbuka jambo hilo kama si Juventus na Paris Saint-Germain zitakazohitaji huduma yake kwa sababu Barcelona na Real Madrid hakuna timu itakayokuwa tayari kumsajili na kwenda kumlipa mshahara huyo unaoanzia Pauni 290,000 kwa wiki na kuendelea.

Staa wa Kibrazili, Neymar atakuwa na kazi moja tu ya kukubali kushusha mshahara wake anaolipwa kwa sasa wa Euro 500,000 kwa wiki kama anataka kuondoka PSG kwa sasa kwa sababu ni jambo gumu kupata timu itakayotuwa tayari kumsajili na kwenda kumlipa mshahara huo au unaozidi kiwango hicho. Si Man United, Man City, Real Madrid, Barca wala Juve zenye uwezo wa kumsajili mchezaji huyo kwa mshahara wake anaolipwa huko Paris.

Dili hizo za mishahara ndizo zinazotajwa kuwa vikwazo kwa wengi kunaswa na timu nyingine huku wachezaji wenyewe wakigoma kushusha mishahara yao ya sasa!