Tenga: Kufuzu kwa Stars kumeniondolea aibu

Muktasari:

 

  • Tanzania imefuzu kwa mara ya kwanza kwa Afcon tangu ilipofanya hivyo mwaka 1980 nchini Nigeria

Dar es Salaam. Nahodha wa zamani wa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Leodegar Tenga amesema kuwa kufuzu kwa timu hiyo katika fainali za Afcon nchini Misri kumemfariji na kumuondolea aibu ya siku nyingi.

Tenga ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT) na mjumbe wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (Caf) alisema kuwa mara kadhaa amekuwa akisimamia mashindano ya Afcon bila ya kuwa na timu ya Tanzania, jambo ambalo lilimuudhunisha sana.

Alisema kuwa baadji ya wasimamizi wa vituo wa mashindano ya Afcon wamekuwa wakifanya kazi hiyo huku wakiwa na timu zao zilizofuzu kinyume na Tanzania.

“Sasa nina cha kujivunia katika mashindano ya Afcon, timu yangu imefuzu name nitakuwa na cha kujivunia baada ya kuwa kimya kwa miaka mingi sana,” alisema Tenga.

Tenga ambaye pia ni miongoni mwa wachezaji waliocheza fainali za Afcon mjini, Lagos, Nigeria alisema kuwa anajivunia baadhi ya wachezaji waliokuwa kuwa kwenye program ya vijana iliyoanzishwa na TFF iliyokuwa chini yake wameweza kuleta mafanikio kwa Taifa.

“Hii nayo ina nivunia sana, wachezaji wengi walikuwa katika timu za vijana ambazo zilianza kupata umaarufu na kuhimarisha programu hiyo chini ya uongozi wetu hii imenipa faraja sana,” alisema Tenga.

Alisema kuwa hatua ambayo Tanzania imefikia ni ya kujivunia sana kwani imewapa faraja Watanzania ambao ni mashabiki wakubwa sa mpira wa miguu.

“Tunachotakiwa kufanya sasa ni kujiandaa vizuri na kuweka historia kwa kufanya vyema katika mashindano ya Misri ili kuendeleza hamasa zaidi,” alisema.

Alisema kuwa wachezaji wanatakiwa kujivunia hatua hii kwani ni historia kubwa sana katika maisha yao ya mpira na haitafutika.