Tazama utabiri wa mabondia kuhusu Wilder,Tyson Fury

Muktasari:

Hawa hapa mabondia wa ngumi za uzito wa juu wa zamani na sasa ambao, wametoa utabiri wao nani atachapwa kati ya Wilder na Fury.

LAS VEGAS ,MAREKANI . LAZIMA pachimbike. Deontay Wilder na Tyson Fury Jumamosi tu hapo watapanda ulingoni huko Las Vegas kuonyeshana ubabe, huku dunia ya wapenzi wa mchezo wa masumbwi ikifuatilia pambano hilo kwa karibu sana.

Pambano hilo la nguvu la uzito wa juu linatarajia kuvuta hisia za wengi na hivyo kufanya mabondia kibao kutoa maoni yao kuona nani ataibuka na ushindi siku hiyo.

Hawa hapa mabondia wa ngumi za uzito wa juu wa zamani na sasa ambao, wametoa utabiri wao nani atachapwa kati ya Wilder na Fury.

Anthony Joshua: Tyson Fury anashinda

Joshua aliambia Pep Talk UK: “Nadhani Fury atashinda. Nimesema hivyo. Nadhani alikaribia kufanya hivyo kwenye pambano lao la kwanza, hivyo hawezi kukosea tena safari hii akikutana na Wilder.

“Alikaribia kufanya hivyo kwenye pambano la kwanza lililomalizika kwa sare. Sasa nadhani Tyson Fury atarekebisha makosa ya mwanzo na kwenda kushinda pambano hilo.”

Bondia Anthony Joshua ni bingwa wa uzito wa juu wa WBA, IBF na WBO.

Mike Tyson: Ampa ushindi Tyson Fury

Tyson aliambia BT Sport: “Siku zote namuunga mkono kwa sababu alipewa jina langu. Hiyo ipo sawa, hakuna makosa hapo sivyo? Lazima niwe upande wake. Haijalishi ngumi nzito kiasi gani unapiga, siku zote ni ngumu sana kumpiga mtu anayevumilia ngumi muda wote na hayupo tayari kukubali yaishe. Litakuwa pambano tamu na lenye mvuto mkubwa kwa sababu mabondia wote watakuwa na kitu watakachotaka kuthibitisha ndani ya ulingo. Namtakia kila la heri Tyson Fury, mimi siku zote ni shabiki wake.”

Tyson Fury na Mike Tyson waliwahi kukutana ana kwa ana mwaka jana.

David Haye: Deontay Wilder atashinda

Haye aliambia BT Sport: “Fury alipigana vizuri kwenye pambano la kwanza wakati huo Ben Davison alikuwa kwenye kona yake. Safari hii Ben hatakuwapo kwenye kona yake. Kwenye pambano lililopita, alipasuliwa mara kadhaa jichoni. Hilo linaweza kutokea tena safari hii na kwamba, haionekani kama ataweza kuendelea kupigana akiwa na jicho moja. Kumpiga Deontay Wilder tu ukiwa na macho mawili ni shughuli. Naona kabisa Deontay Wilder atashinda pambano hili bila ya shida yoyote.

David Haye ni bingwa wa zamani wa dunia wa WBA kwa uzito wa juu.

Dillian Whyte: Inategemea na mpango wa mechi

Whyte alisema: “Nadhani Fury atapiga ngumi nyingi na kila kitu kuwa upande wake.

“Kama atajaribu kutafuta KO, atalazimika kupiga ngumi za kweli kumtuliza Deontay Wilder. Akipigana vinginevyo basi mambo yanaweza kuwa kinyume chake. Kwa kusema hilo, Wilder si mtu kawaida, kuna vitu amekuwa akivifanya kwa ubora pia. Hii mechi itamalizwa kwa mpango wa kila bondia kuhusu pambano lenyewe. Kuna mambo mengi sana yatatokea. Subiri tuone.”

Dillian Whyte anashikilia kwa muda mkanda wa WBC.

Charles Martin: Deontay Wilder atashinda kwa KO

Martin aliambia Fight Hub: “Fury atapiga ngumi nyingi kuliko mpinzani wake, atafanya mambo yake, lakini Wilder atampiga ngumi moja tu ya mkono wa kulia na hapo pambano litakuwa limekwisha. Amekuwa akifanya hivyo mara nyingi, anapiga KO za ngumi moja moja tu. Nimekuwa nikijifunza mengi sana kwa Wilder. Kwa kutazama rekodi zake, hili ni pambano lake la pili dhidi ya bondia huyo, hivyo atahitaji kuweka mambo yake sawa. Itakuwa ile balaa kwa ngumi yake ya mkono wa kulia.”

Charles Martin ni bingwa wa zamani wa IBF uzito wa juu.

Wladimir Klitschko: Tyson Fury atashinda kwa pointi

Fury aliambia The National: “Ama Wilder atakayempiga kwa KO Fury au Fury kushinda kwa pointi. Binafsi namheshimu sana Wilder, aliwahi kuwa kwenye kambi yangu ya mazoezi, tumeshiriki pamoja raundi kadhaa ulingoni. Ni bondia mzuri na ni makini pia. Kwa idadi ya KO nyingi alizonazo, inakuonyesha si mtu ambaye unaweza kumchezeachezea kirahisi kwenye pambano la uzito wa juu. Lakini, ninachokiona, naona ni Fury atakayekwenda kushinda, najua atalifanya hilo.”

Wladimir Klitschko ni bingwa wa zamani wa uzito wa juu duniani.

Oleksandr Usyk: Tyson Fury atashinda

Usyk aliambia Ren TV: “Nilimpa nafasi Tyson Fury kwenye pambano la kwanza. Kwenye pambano la pili bila ya shaka nitaendelea kuwa upande wake. Amekuwa na ujuzi zaidi kuliko Wilder. Lakini, Wilder ni mtu asiyetabirika, anaweza kukuchapa ngumi ukashindwa kurudi tena ulingoni muda wowote ule.”

Oleksandr Usyk hivi karibuni amepandishwa kucheza ngumi za uzito wa juu.

Lennox Lewis: Deontay Wilder yupo vizuri

Lewis aliambia Boxing Social: “Nadhani litakwenda kuwa pambano la aina yake, bondia dhidi ya mpiga ngumi.

“Kuna watu watakuwa upande wa nguvu na kuna wengine watakuwa upande wa ngumi, mimi napenda mapambano ya aina hiyo.

“Hakuna anayefahamu hasa nini kitakwenda kutokea, nani atafanya makosa yatakayomgharimu? Nani hatafanya makosa. Hakuna utabiri. Siwezi kusema kwa sasa, ila Deontay yupo vizuri.”