Tayari Nduda kaanza tambo!

Muktasari:

Licha ya kuachwa na Simba, alikiri kuna ujuzi ambao ameupata kwa makocha na utamsaidia kwenye maisha yake mapya akiwa na Ndanda.

KIPA Said Mohamed ‘Nduda’ kesho Jumapili anajiunga na timu yake mpya ya Ndanda FC, baada ya kutemwa kwenye mpango wa Kocha Patrick Aussems, aliyebaki na makipa watatu, Aishi Manula, Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Salimu aliyepandishwa kutoka timu ya vijana.

Nduda aliliambia Mwanaspoti alikuwa na sababu za kutojiunga na Ndanda FC kwa muda mwafaka na sasa kila kitu kipo freshi na ataanza kufanya yake.

“Mambo ya timu ni mengi tofauti na mashabiki wanavyoangalia, nimeondoka Simba sio kwa sababu ya Manula na Dida wamenizidi uwezo, hapana viwango vyetu ni vile vile isipokuwa mwingine anaweza kuwa mzuri na mipira ya kona, penalti yaani kifupi kila mtu ana vionjo vyake. “Nina imani Ndanda itanirejesha tena kwenye piki mpaka kupata namba ndani ya kikosi cha Taifa Stars, nitacheza na sasa ninafanya mazoezi ya nguvu,” alisema Nduda.

Licha ya kuachwa na Simba, alikiri kuna ujuzi ambao ameupata kwa makocha na utamsaidia kwenye maisha yake mapya akiwa na Ndanda.