Tatizo hapa ni uofisa habari tu!

Tuesday August 13 2019

 

Agosti 4, 2019 itaingia kwenye historia kwamba klabu ya Yanga iliandaa kwa mara ya kwanza tukio lao la Siku ya Mwananchi, na kufana.

Wiki moja baadaye, Yanga haohao wakatupa karata yao ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuwakaribisha Township Rollers kutoka Botswana.

Ukitazama majukwaa kwenye Siku ya Mwananchi na siku ya mechi ya Ligi ya Mabingwa unaweza ukadhani haya yalikuwa matukio yanayozihusu klabu mbili tofauti.

Siku ya Mwananchi, watu walijaa vilivyo, lakini siku ya mechi ya Ligi ya Mabingwa majukwaa yalikuwa tupu.

Mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo ukazuka mjadala wa kinachokosekana Yanga kiasi cha watu kushindwa kujitokeza uwanjani.

Wengi wa waliotoa maoni yao, wakamtupia lawama ofisa habari wa klabu hiyo, Dismas Ten.

Advertisement

Unaweza ukajiuliza Ten anahusikaje na watu kutoenda uwanjani? Kama ofisa habari alitakiwa afanye nini watu waende uwanjani?

Kazi ya uofisa habari ni kutoa taarifa za klabu kama anavyopewa na wakuu wake. Moja ya taarifa hizo ni ratiba za mechi. Kwani ina maana mashabiki wa Yanga hawakujua kama timu yao itacheza na Township Rollers?

Katika hali ya kiueledi, kazi ya kuwahamasisha watu kwenda uwanjani ni ya idara ya masoko na matangazo.

Watu wa masoko walipaswa kuiuza mechi hii kwa mashabiki wao ili waende kwa wingi uwanjani.

Udhaifu wa idara ya masoko unageuka kuwa msala kwa Dismas Ten. Unajua kwa nini? Ten hatakiwi Yanga.

KIVIPI?

Kuna mambo mengi sana yanaendelea Yanga yakihusishwa na viongozi waliopita, Ten akiwa peke yake aliyebaki.

Kuna mizengwe mingi inayotengenezwa ili kuhakikisha kung’olewa kwa Ten kunakamilika. Kugoma kwa akina Yondani, Juma Abdul na Andrew Vicent wakishinikiza malipo yao kutokana na mikataba iliyopita kunahusishwa na Ten na viongozi wenzake waliokuwepo katika awamu iliyopita.

Wanaosuka zengwe hili wanatumia udhaifu wa mifumo katika vilabu vyetu ili kufanikisha mipango yao.

Kwa mfano, kuna taarifa kwamba viongozi wanasema hawawezi kuwalipa wachezaji wale kwa sababu hakuna nyaraka zozote zinazoonyesha kwamba wanaidai klabu.

Sasa wapika propaganda wameunganishia hapohapo kwamba kugoma kwa wachezaji hao hakutokani na madai, bali ni hujuma inayofanywa na viongozi waliopita ili kuwadhoofisha viongozi wa sasa. Na kwa kuwa Ten amebaki, anaonekana yeye ndio anatumika kutoa udhaifu wa ndani kwa viongozi waliopita, yaani anauza ramani ya vita.

SABABU

Kuna watu walipigana sana kuhakikisha uongozi wa sasa wa Yanga unaingia madarakani. Watu hao ambao taaluma zao ni uandishi wa habari, wanakitaka kiti cha Ten, na ndio hao wanaoanzisha hizi propaganda.

Watu hawa wako karibu sana na uongozi wa Dk Mshindo Msolla na wanajitahidi kwa kila namna kuonyesha wanavyofaa kwa nafasi hiyo kuliko Ten.

Ukipata nafasi ya kukutana nao utawasikia wakisema “Ten hana lolote, sema tu alibebwa na ndugu yake Clement Sanga wakati akiwa makamu mwenyekiti”.

Kwa hiyo kila kitu ambacho hakitaenda vizuri Yanga, kikwazo kitaonekana ni Dismas Ten tu, hadi ang’oke.

Hapa ndipo nakumbuka hotuba ya Edward Lowassa siku akijiuzulu uwaziri mkuu kwa kashfa ya Richmond, alisema, “tatizo ni uwaziri mkuu’. Na hapa kwa Ten, tatizo ni uafisa habari tu!

Advertisement