Tanzanite ipo tayari Cosafa

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikipangwa kundi moja na timu za Zimbabwe na Botswana kwenye mashindano ya wanawake ya Cosafa, kocha Bakari Shime wa timu ya taifa ya wanawake (Tanzanite), Bakari Shime amesema wapo tayari kuikabili timu yoyote.

Mashindano hayo ya vijana chini ya miaka 17 yataanza Novemba 3 hadi 14 kwenye uwanja wa Nelson Mandela Bay nchini Afrika Kusini.

Droo ya mashindano hayo imechezeshwa jana na Tanzania kupangwa kundi C na Zimbabwe na Botswana.

Akizungumzia kundi hilo, kocha Shime alisema hana wasiwasi nalo kwani walijipanga kucheza na timu yoyote.

“Tuko tayari kupambana, tunahitaji kufanya vizuri na hatua hofu na timu yoyote tutakayokutana nayo, tunaamini tutafanya vizuri,” alisema kocha huyo.

Alisema wanafahamu ugumu na ushindani wa mashindano hayo, lakini anaamini kikosi chake kitafanya vizuri.

“Lengo letu ni kurejea na ubingwa, tutakwenda Afrika Kusini kupambana kwa ajili ya ubingwa na si vinginevyo.

“Hatutajali tunacheza na timu gani au ina rekodi gani, kwani rekodi gani kisoka, ila tutambana kwa uwezo na kiwango chetu kwa ajilin ya kusaka mafanikio na ubingwa,” alisema.

Tanzania itafungua diimba Novemba 4 dhidi ya Zimbabwe na Novemba 7 itacheza mechi ya mwisho ya makundi na Botswana mechi zote zitachezwa kwenye uwanja wa Wolfson.

Kama itashinda itafuzu kucheza nusu fainali itakayochezwa Novemba 12 na Novemba 14, itakuwa ni fainali ya mashindano hayo uwanjani hapo.

Timu hiyo itarejea nchini Novemba 15, ambapo kwa mujibu wa kocha Shime, wanatarajia siku hiyo kurejea wakiwa na ubingwa wa mashindano hayo.

Katika droo ya makundi mengine kwenye mashindano hayo, bingwa mtetezi, Afrika Kusini wamepangwa Kundi A na timu za Eswatini, Comoro na Angola, wakati Kundi B lina timu za Zambia, Malawi na Lesotho.