Tanzanite Queens yatema cheche ligi ya wanawake

Muktasari:

Msimu uliopita timu Tanzania Queens ilitolewa hatua ya nusu fainali kwa kupigwa 3-1 na Simba Queens na kuzima ndoto zao.

LIGI Daraja la Kwanza ya Wanawake imeendelea kushika kasi huku Tanzanite kutoka Arusha ikiendelea kufanya vyema baada ya juzi Jumatano kuiangushia furushi la mabao 4-0 Allans Queens ya Dodoma na kukaa kileleni mwa kundi hilo ikiwa na pointi tisa.
Mabao ya Tanzanite katika mchezo wa juzi Jumatano yaliwekwa kambani na Agness Pallangyo aliyetupia dakika ya 15, 17, 25 na 41, hivyo kumfanya kufikisha mabao matano katika michezo mitatu waliyocheza, kwani katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Singida alifunga bao moja na kuiwezesha timu hiyo kuondoka na ushindi wa mabao 2-1.
Katika mchezo wa pili waliocheza na Abeehe Bha Kyela pia waliibuka kidedea kwa kuichapa mabao 2-1 kwa mabao ya Maria Peter na Hawa Suleiman.
Leo Ijumaa Tanzanite itavaana na Mapinduzi Queens ya Njombe, huku Kocha wa timu hiyo, Abdallah Juma akisema lengo lao ni kupata nafasi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
"Hakuna sababu itakayotufanya tushindwe kutimiza malengo yetu, tayari tumewasoma wapinzani wetu na kujitathimini jinsi tulivyo," alisema Juma.