Tanzania yatwaa ubingwa Copa Coca-Cola Afrika

Muktasari:

Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa M-Pesa Foundation Academy, Thika, Tanzania ilianza kwa kasi na Nyerere akifunga mabao matatu (hatrick) katika kipindi cha kwanza.

Thika, Kenya. Tanzania imeicharaza Zimbabwe kwa mabao 6-2 kutwaa ubingwa wa Copa Coca-Cola wa Afrika kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 16.

Mbali ya kutwa ubingwa huo kwa kishindo, mshambuliaji wa Tanzania, Paul Nyerere aliikubuka mfungaji bora wa mashindano hayo na kuzawadiwa tuzo ya kiatu cha dhahabu.

Katika mechi hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa M-Pesa Foundation Academy, Thika, Tanzania ilianza kwa kasi na Nyerere akifunga mabao matatu (hatrick) katika kipindi cha kwanza.

Hatrick hiyo ilikuwa ya pili kwa Nyerere ambapo katika mchezo dhidi Uganda, alifunga mabao matatu katika ushindi wa mabao 6-2.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Pindi Chana aliikabidhi Tanzania kombe na zawadi ya kiatu cha dhahabu kwa Nyerere.

Mbali ya Nyerere kufunga mabao matatu, wachezaji wengine walioifungia Tanzania katika mashindano hayo ni Ndile Haruni, Rai Mohambi na Boniface Raphael.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Abel Mtweve alisema kuwa haikuwa kazi rahisi kutwaa ubingwa huo kutokana na ushindani mkali kutoka kwa wapinzani.

Mtweve alisema kuwa siri kubwa ya mafanikio hayo ni maandalizi bora kutoka kampuni ya Coca-Cola na moyo wa kujituma kwa wachezaji wake.

“Timu kufungwa mabao mengi si kuwa ni dhaifu, ni kuzidiwa mbinu, wachezaji wangu hawajaanza vizuri mashindano baada ya kufungwa na Zambia mabao 2-0, ilitokana na uchovu, tulipata muda wa kupumzika na kuanza kutoa dozi,” alisema Mtweve.

Alisema kuwa timu yake imestahili ushindi kutokana na mchezo mzuri wenye kuvutia.

Kipa wa timu hiyo, Chuma Ramadhan ameacha historia kubwa katika mashindano baada ya kuokoa hatari nyingi.

Mwakilishi kutoka Coca-Cola Tanzania, Pamela Lugenge alisema, "Ninawapongeza sana vijana wetu, wameonyesha bidii kubwa na sasa tunarudi nyumbani na kombe,"alisema.

Coca-Cola wadhamini wakuu wa mashindano hayo katika ngazi zote za kitaifa hadi kimataifa.