Tanzania yapewa mkwanja mnene

Muktasari:

  • Habari njema kwa wacheza Tenisi nchini ni kwamba kituo hicho kitapokea mchezaji kutoka sehemu yoyote nchini ili mradi awe na kipaji cha mchezo huo na hapo itasaidia kuongeza ushindani kutoka kwa nyota hao wa mataifa ya nje.

MAMBO yameanza kuwanyookea wachezaji Tenisi wa Tanzania ambao siku si nyingi utaanza kuwasikia kwenye anga nyingine kabisa.

Iko hivi, Chama cha Tenisi cha Kimataifa (ITF) kimekipa Chama cha Tenis Tanzania (TTA) kitita cha dola 20,000 (zaidi ya Sh 44 Milioni) kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mafunzo (training center).

Habari njema kwa wacheza Tenisi nchini ni kwamba kituo hicho kitapokea mchezaji kutoka sehemu yoyote nchini ili mradi awe na kipaji cha mchezo huo na hapo itasaidia kuongeza ushindani kutoka kwa nyota hao wa mataifa ya nje.

“Ujenzi wa kituo hicho kinatarajia kuanza mapema mwezi huu na kitakamilika Januari mwishoni kama kitakwenda vizuri kulingana na maelezo ya wataalam wa kituo hicho,” alisema rais wa TTA, Denis Makoyi.

Alisema ujenzi huo utafanywa na BQ Contractors ambao wataboresha viwanja vinne vya mchezo huo vilivyopo katika klabu ya Gymkhana ya jijini Dar es Salaam, uwanja ambao unatumika zaidi katika michezo hiyo.

Meneja Maendeleo na Biashara wa BQ Contractors, Hilu Bulla alisema ujenzi huo utahusisha ujenzi wa kituo na viwanja kwa ufasaha mkubwa ili kuvutia wadau wengine katika kuwekeza kwenye michezo.

Naibu Katibu Mkuu wa TTA, Inger Njau alisema zoezi la mafunzo litahusisha vijana kati ya miaka 10 hadi 18 na linatoa fursa kwa vijana wote wenye vipaji vingi kutoka mikoa mbalimbali na hata nje ya nchi.

Kituo hicho kitasimamiwa na Kocha wa Tenisi nchini, Salum Mvita pamoja na wadau wengine wa kuhakikisha lengo la mchezo huo unazidi kufika mbali hapa nchini na kufanya vyema kwenye mashindano.