Tanzania kicheko kimtindo, Senegal kumkosa kiungo N’Doye

Muktasari:

  •   Senegal itafungua fainali za AFCON2019 hapo Juni 23 kwa kucheza dhidi ya Tanzania kabla ya kuivaa Algeria na Kenya  

Dar es Salaam. Adui muombe njaa! Ndicho unachoweza kusema kwa upande wa Tanzania baada ya kuwepo kwa taarifa kuwa kiungo wa Senegal na Angers, Cheikh N’Doye anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa goti na kuondoa uwezekano wa kucheza AFCON.

Tanzania imepangwa Kundi C pamoja na Senegal, Algeria na Kenya katika fainali hizo za Afcon zitakazofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19, 2019

Kiungo huyo mwenye miaka 33, alipata majeruhi hayo wakati wa mchezo wa kirafiki dhidi ya Mali uliofanyika  Machi, hata hivyo ilionekana kuwa siyo tatizo kubwa baada ya vipimo sasa atalazimika kufanyiwa upasuaji jambo litakalomweka nje kwa muda mrefu.

N’Doye ni nguzo muhimu katika kikosi cha kocha Aliou Cisse hiyo ni kutokana na kiungo huyo kucheza mechi mbili za Senegal katika Kombe la Dunia lililopita. Pia ni mchezaji mwenye uzoefu zaidi katika kikosi chao kilichojaa vijana wengi.

Endapo N’Doye atakosa fainali hizo atafungua milango kwa Assane Diousse kurejea kikosini, pamoja na kuwa na msimu mgumu katika klabu ya Chievo Verona anayocheza kwa mkopo akitokea St Etienne.

Akiwepo au asipokuwepo kiungo huyo, Senegal itafungua fainali za AFCON2019 hapo Juni 23 kwa kucheza dhidi ya Tanzania kabla ya kuivaa Algeria na Kenya katika moja ya makundi magumu zaidi katika mashindano hayo.