Tambwe sasa anafanya kweli

STAA anayeshikilia rekodi ya mabao kwa nyota wa kigeni, Amissi Tambwe ameamua kufanya kweli baada ya kuanza maandalizi ya kuwapiga watu ubeche wakati akijiandaa kufanya sherehe ya ndoa dhidi yake na Raiyan ‘Ray Sharp’.

Inaelezwa sherehe hizo zitachukua siku tano kufanyika na ndugu, jamaa na rafiki sambamba na mashabiki wa Yanga wajiandae tu, kwani inaelezwa Novemba 7 ndio shughuli zinaanza kwa kitchen party pale Kariakoo kisha Nov 9 ndio harusi yenyewe itakayofungwa Buruguni Malapa.

Usiku wa Novemba 10, mitaa ya Ilala kutakuwa na sherehe ambayo wameipa jina la Usiku wa Zawadi na baada ya hapo itafuata sherehe yenyewe kubwa na hiyo ni upande wa mwanamume itafanyika Burundi nyumbani kwa Tambwe na itatategemea kipindi ambacho Tambwe atakuwa mapumziko.

Wawili hao walikutana miaka minne iliyopita na kujaaliwa kupata mtoto wa kiume, Ayman.