Taifa ni Stars vicheko tu

Muktasari:

Tanzania ilipenya hatua ya makundi baada ya mchezo huo kuamuliwa kwa penalti 3-0, zilizofungwa na Erasto Nyoni, Himid Mao na Gadiel Michael, wakati penalti za Burundi zilizopigwa na Saido Berahino na Gael Bigirimana ziliota mbawa huku ile ya Omar Ngando ikiokolewa kishujaa na kipa mzoefu Kaseja.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, jana alimkabidhi Juma Kaseja zawadi ya Sh. 10 milioni baada ya kipa huyo kuokoa penalti dhidi ya Burundi na kuisaidia Taifa Stars kuingia katika hatua makundi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2022.

Makonda alitoa zawadi hiyo kama Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa ya Taifa Stars kwa kipa huyo ambaye kwa wengi alionekana kuwa ndiye nyota mchezo.

Stars juzi Jumapili ilifanya kile ambacho Watanzania walikuwa wanakitaka baada ya kuiondosha Burundi kwa penalti 3-0.

Mchezo huo ulilazimika kutumia dakika 120 baada ya sare ya mabao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa kulingana na sare ya bao 1-1 katika mechi yao ya kwanza kule Burundi. Stars walitangulia kupata bao katika dakika 29 kupita Mbwana Samatta lakini, wageni walicharuka na kusawazisha katika dakika ya 45 kupitia, Fiston Razak.

Tanzania ilipenya hatua ya makundi baada ya mchezo huo kuamuliwa kwa penalti 3-0, zilizofungwa na Erasto Nyoni, Himid Mao na Gadiel Michael, wakati penalti za Burundi zilizopigwa na Saido Berahino na Gael Bigirimana ziliota mbawa huku ile ya Omar Ngando ikiokolewa kishujaa na kipa mzoefu Kaseja.

Shangwe, furaha na vicheko ni kati ya mambo yaliyotawala kwenye Uwanja wa Taifa juzi.

Haya hapa ni mambo 8 yaliyotingisha ndani na nje mchezo huo.

1. Kaseja penalti

Uwezo wa Kaseja katika kupangua penalti uliendelea kujidhihirisha pale alipofuta penalti ya kwanza ya Burundi iliyopigwa na Ngando na kuwavuruga wageni hao.

Ni mwezi mmoja tu tangu Tanzania iing’oe Kenya kwa mikwaju ya penalti katika kusaka tiketi ya kushiriki michuano ya Chan, Kaseja akiokoa penalti tena ya upande ule ule wa kushoto kama ilivyokuwa juzi.

2. Uamuzi mgumu wa Ndayiragije

Wengi hawakukubaliana na uamuzi wa kocha Etienne Ndayiragije kumrejesha Kaseja kwenye kikosi hicho baada ya miaka mingi kupita ambayo Aishi Manula na makipa wengine walitamba kwenye nafasi hiyo. Hata hivyo, uamuzi huo umeonekana sahihi baada ya kipa huyo veterani kugeuka shujaa wa taifa.

Uamuzi mwingine mgumu wa Ndayiragije juzi ambao awali haukueleweka kwa wengi ulikuwa ni kuwaanzisha, Idd Seleman ‘Nado’, na Hassan Dilunga ‘HD’, ambaye hana uhakika na namba kikosini Simba huku akimuacha nje Farid Musa, ambaye amekuwa akianza Stars hata katika fainali za Afcon 2019.

3. Harmonize fungate taifa

Kwa desturi za Kitanzania mtu anapofunga ndoa hupenda kwenda sehemu tulivu kwa siku kadhaa, lakini nyota wa Bongofleva, Rajab Abdul Kahali ‘Harmonize’ ambaye siku moja kabla ya mchezo huo alitoka kufunga pingu za maisha na mchumba wake raia wa Italia, Sarah Michelotti, alikuwapo uwanjani kuwapa sapoti Stars akithibitisha mapenzi yake kwa taifa lake.

Harmonize aliongoza shangwe la mashabiki kutokea jukwaani na baada ya mechi aliingia ndani ya uwanja pembeni ya dimba kushangilia pamoja na wachezaji.

4. Hamasa ya mashabiki

Siyo jambo rahisi kuujaza Uwanja wa Taifa unaopokea mashabiki 60,000 hasa kwa mechi za timu ya taifa, lakini juzi kulikuwa na umati mkubwa wa mashabiki wakiwamo mastaa kadhaa waliojitokeza, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ akiwa miongoni mwao.

5. Kuumia kwa Samatta

Katika matukio adimu sana, nahodha na mfungaji wa bao la Stars, Mbwana Samatta alipumzishwa baada ya dakika 15 za kwanza za nyongeza na alitoka akiwa amefungwa barafu kwenye goti la mguu wake wa kulia. Nafasi ya Samatta, ilichukuliwa na Himid Mao ambaye alikuwa mmoja wa wapiga penalti.

Katika ukurasa wake wa Insta, Samatta ambaye aliondoka kurudi Ubelgiji baada ya mechi, aliandika: “Japo njia ya ushindi ilikuwa ngumu lakini mwisho tulipata tulichokitaka, kama ‘captain’ nikiwakilisha wachezaji wenzangu pamoja na benchi la ufundi tutakuwa wachoyo wa fadhila tusipowashukuru nyote mliojitokeza katika michezo hii miwili dhidi ya Burundi, sapoti yenu ilitusukuma pale ambapo kulilega, na matokeo haya ya kufuzu hatua ya makundi tunaya-’dedicate’ kwenu Watanzania wote mnaoisapoti timu ya Taifa kwa moyo wa dhati, hata wale ambao hawakupata bahati ya kufika uwanjani, na popote walipokuwa waliomba ushindi kwa moyo mmoja na pia kwa wote ambao kwa njia moja ama nyingine walitumia njia yoyote kuhamasisha wengine kuisapoti timu yao. Asante sana. Viva Taifa Stars. Haya wote kunyweni koka bili ya kwangu.”

6. Ndayiragije kuwatoa nduguze

Kazi ya ukocha ni sawa na mchezaji, popote kambi. Matokeo ya juzi yalikuwa ni tamu-chungu kwa Ndayiragije kwani amefanikisha ajira yake ya ukocha Taifa Stars, lakini anaugulia ndani kwa ndani kulitoa taifa lake katika ndoto za kufika mbali katika kufuzu kwa Kombe la Dunia.

7. Manahodha wanacheza Ubelgiji

Nahodha wa Burundi, Berahino aliyepata kucheza kwenye Ligi Kuu ya England akiwa na West Brom na Stoke City, hivi sasa anakipiga Ubelgiji katika timu ya S.V Zulte Waregem, ligi moja na nahodha wa Stars, Mbwana Samatta wa Genk. Tena Berahino alifunga bao moja katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Genk ya Samatta zilipokutana mapema msimu huu.

8. Makipa wa KMC

Kipa Jonathan Nahimana aliingia katika dakika za lala salama, juzi jambo lililomaanisha kwamba makipa waliopigiwa penalti wote wanatokea klabu moja ya KMC.