Taifa Stars yasubiria vigogo 14

Muktasari:

Kanda ya Afrika Magharibi ndio inayotoa idadi kubwa ya timu kwenye mashindano ya Chan ambapo ina nafasi ya kupeleka nchi tano ikifuatiwa na kanda za Afrika Mashariki na Kati na ile ya Kusini ambapo kila moja itawakilishwa na nchi tatu

WAKATI timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ikiwa ya kwanza kufuzu Fainali za Mataifa Afrika kwa Wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) zitakazofanyika mwakani ukiondoa wenyeji Cameroon, jumla ya timu 14 zinasubiriwa ili kutimiza idadi ya timu 16 zitazoshiriki mashindano hayo.
Ushindi wa mabao 2-1 ugenini dhidi ya Sudan jana Ijumaa usiku, umeifanya Stars kufuzu kwa faida ya bao la ugenini ikiwa ni baada ya kufungwa bao 1-0 kwenye mchezo wa kwanza nyumbani na hivyo kuifanya iungane na Cameroon ambayo imetinga moja kwa moja kwenye fainali hizo kama timu mwenyeji.
Timu hizo 14 zilizobakia ili kukamilisha idadi ya nchi 16 zitakazoshiriki fainali hizo mwakani, zitapatikana kupitia mechi nyingine za marudiano ambazo  zitachezwa katika nchi mbalimbali leo Jumamosi na kesho Jumapili.
Utaratibu ulivyo
Kanda tano za soka barani Afrika kila moja hutoa wawakilishi kulingana na idadi ambayo imepangwa na Shirikisho la Soka Afrika kwa kila kanda kutoka kwenye mashindano hayo.
Kanda hizo ni Kaskazini, Magharibi, Afrika Mashariki na Kati, Kanda ya Kusini mwa Afrika na Kanda ya Afrika ya Kati.
Nani kuzifuata Stars na Cameroon?
Kanda ya kwanza ambayo ni ile inayoundwa na nchi zinazunda Shirikisho la Soka Kaskazini (UNAF) ambayo yenyewe  ina nafasi mbili za uwakilishi kwenye Fainali za Chan.
Baada ya kutoka sare ya bila kufungana kwenye mechi ya kwanza ugenini dhidi ya Algeria, Morocco itakayokuwa nyumbani inahitaji ushindi wa aina yoyote katika mchezo huo utakaochezwa leo na ikiwa itapoteza au kutoka sare ya mabao, itaaga mashindano hayo huku matokeo ya suluhu yakilazimisha mechi hiyo kuamriwa kwa mikwaju ya penati.
Timu nyingine ambayo itakamilisha idadi ya nchi mbili zitakazofuzu upande wa ukanda huo itapatikana kupitia mchezo wa marudiano baina ya Tunisia na Libya.
Katika mchezo wa kwanza, Tunisia iliibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kesho Jumapili itakuwa ugenini ikihitaji sare au ushindi ili isonge mbele.
Afrika Magharibi (WAFU)
Shirikisho la Soka Afrika Magharibi (WAFU) lenyewe lina nafasi tano ambazo zinapatikana kupitia kanda mbili ndogo zilizogawanywa ambazo ni WAFU A na WAFU B.
Kanda ya WAFU A ambayo itatoa timu mbili, itakuwa na mechi zitakazokutanisha Guinea na Senegal na ile ya Mali dhidi ya Mauritania.
Katika mechi za kwanza, Senegal iliibuka na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Guinea wakati Mauritania ililazimishwa sare ya bila kufungana nyumbani na Mali.
Kanda ndogo ya WAFU B yenyewe inatoa timu tatu na kutakuwa na mechi tatu mwishoni mwa wiki hii kuanzia leo ambapo Nigeria itacheza na Togo huku kesho kukiwa na mechi baina ya Ivory Coast na Niger huku Burkina Faso ikicheza na Ghana.
Togo ipo ugenini dhidi ya Nigeria ikihitaji sare au ushindi wa aina yoyote baada ya kushinda mabao 4-1 nyumbani, wakati mchezo wa kwanza ugenini kwa Ivory Coast ambayo itaialika Niger, ilichapwa mabao 2-0.
Burkina Faso watakuwa nyumbani kuialika Ghana wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ugenini kwenye mechi ya kwanza.
Kanda ya Afrika ya Kati (UNIFFAC)
DR Congo itakuwa nyumbani kuwaalika Afrika ya Kati wakiwa na mtaji wa ushindi wa mabao 2-0 ugenini wakati mechi nyingine itakuwa ni kati ya Guinea ya Ikweta na Congo ambazo zilitoka sare kwenye mechi ya kwanza.
Kanda ya Kusini mwa Afrika (Cosafa)
Zimbabwe iko kwenye nafasi nzuri ya kufuzu Chan ikihitaji ushindi au sare kwenye mechi yake ya ugenini dhidi ya Lesotho baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 nyumbani, wakati Madagascar iliyoshinda bao 1-0 nyumbani leo itakuwa ugenini dhidi ya Namibia ikitafuta sare au ushindi tu ili isonge mbele.
Mechi nyingine itazikutanisha Zambia na Eswatini ambayo itachezwa leo huko Lusaka. Kwenye  mechi ya kwanza, Zambia ilipata ushindi wa bao 1-0 ugenini
Kanda ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa)
Baada ya Tanzania kuwa ya kwanza kufuzu, Uganda wako kwenye nafasi nzuri ya kufanya hivyo ikiwa wataibuka na ushindi au sare yoyote nyumbani dhidi ya Burundi, wakibebwa na ushindi wa mabao 3-0 ugenini.
Rwanda nayo itakuwa na kibarua cha kulinda ushindi wake wa bao 1-0 ilioupata nyumbani wakati itakapokuwa ugenini dhidi ya Ethiopia, mchezo utakaochezwa leo.