Taifa Stars yajiweka sawa

SAA chache kabla ya mchezo wa kirafiki kati ya Tanzania 'Taifa Stars' dhidi ya Burudi, wachezaji na benchi la ufundi limeamua kujiweka 'sop sop' kidogo.

Wachezaji wa Timu ya Taifa leo wamenyolewa wakati wakijiandaa na mchezo huo wa Kirafiki kwenye Kalenda ya Fifa utakaochezwa Jumapili Oktoba 11, saa 10 jioni Uwanja wa Benjamini Mkapa.

Baadhi ya wachezaji walionekana wakinyolewa ni pamoja na Shomari Kapombe, Simon Msuva sambamba na kocha Etienne Ndayiragije na wasaidizi wake, Suleinam Matola na Juma Mgunda.

Mchezo huo ni wa kwanza kwa timu zote tangu kuzuka kwa janga la corona, Kwenye viwango vya ubora, Taifa Stars iko katika nafasi ya 134 wakati Burundi yenyewe ipo nafasi ya 149.

Tanzania na Burundi mara ya mwisho kukutana ilikuwa ni Septemba 8 katika mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia Stars iliibuka na ushindi wa mikwaju ya penati 3-0 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 kama ilivyokuwa katika mechi ya kwanza iliyochezwa Septemba 4.