Taifa Stars yachangiwa Sh370 milioni

Muktasari:

 Kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu huko Misri, Stars imepangwa kundi C pamoja na timu za Algeria, Kenya na Senegal. 

Dar es Salaam. Takribani Sh370 milioni zimechangishwa katika harambee maalum ya kuichangia timu ya Taifa 'Taifa Stars' inayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazofanyika huko Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19.

Harambee hiyo iliyoongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na kuhudhuriwa na kampuni na taasisi mbalimbali za binafsi na umma ilifanyika kwenye hoteli ya Serena jijini leo asubuhi.

Kiasi hicho ni fedha ambayo ililipwa moja kwa moja na nyingine iliyotokana na ahadi kutoka kwa kampuni na taasisi hizo.

Akizungumza mara baada ya Harambee hiyo kukamilika, Mama Samia alisema harambee imeonyesha mafanikio makubwa na anaamini litakuwa chachu kwa timu ya taifa kufanya vizuri kufanya vyema.

"Kazi tuliyoifanya hapa leo imetusogeza hadi Shilingi 370 milioni. Kampeni hii ni endelevu na itaendelea huko mikoani.

“Kampeni hii naamini inawajaza motisha kwa wachezaji wetu na kwa upande mwingine niwashukuru Watanzania wote kwa muitikio chanya na naomba waendelee kuchanga," alisema Mama Samia.

Miongoni mwa kampuni zilizojitokeza kuichangia Stars ni Mwananchi Communications Limited, Azam Media, ORYX, Benki ya CRDB, Benki ya KCB, Big Bon. Simba Logistics, Afro Oil, Benki ya Posta, TSN Oil, Asas na Mount Meru.