Taifa Stars waitanguliza Cape Verde Uwanja Taifa

Muktasari:

Tanzania inahitaji kushinda mechi hiyo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu kwa Afcon2019 nchini Cameroon

Dar es Salaam. Msafara wa timu ya Taifa ya Cape Verde umekuwa wa kwanza kufika kwenye Uwanja wa Taifa tayari kwa mchezo wake dhidi ya Taifa Stars huku wenyeji wakiingia dakika 12 baadaye.

Cape Verde msafara wao ulikuwa na gari moja tu ambalo ni basi la timu ya Azam FC wanalotumia huku wakiongozwa na pikipiki ya Jeshi la Polisi wa Usalama Barabarani, waliingia uwanja wa Taifa saa 9.20 alasiri na baadaye saa 9.32 msafara wa Stars ulioongozwa na pikipiki ya king'ola na magari matatu uliingia uwanjani hapo.

Kundi kubwa la wachezaji wa Cape Verde walionekana wakiwa na vifaa vya kusikilizia muziki walivyoweka masikioni huku wakionyesha utulivu wa hali ya juu.

Kundi dogo la mashabiki wa Stars walijipanga kando ya basi la timu ya taifa na kuwapigia makofi wachezaji pindi walipokuwa wanashuka garini.