Taifa Stars wababe wa Burundi kwa miaka 49

Wakati mashabiki wa soka wakihesabu saa kuona nani ataibuka mshindi kesho kati ya Taifa Stars na Burundi, Stras itashuka uwanjani ikiwa na rekodi tamu ya kuitambia Burundi kwa miaka 49.

Timu hizo zitakutana kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, katika mchezo wa kirafiki wa kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA).

Taifa Stars itakayoongozwa na nahodha, Mbwana Samatta itaikaribisha Burundi ikiwa na historia ya kuitambia kwa miaka 49 tangu 1971.

Tangu wakati huo, timi hizo zimekutana mara 20 katika mechi za kirafiki, Cecafa, Mataifa ya Afrika na kufuzu Kombe la Dunia na Burundi imeshinda mara tano sawa na asilimia 25, kulinganisha na Stars ambayo imeshinda mara 12 na kutoka sare mara tatu tangu Desemba 5, 1971 hadi Septemba 8, 2019.

Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 kwenye mechi ya kufuzu Kombe la Dunia nyumbani na ugenini, Septemba 4 na 8 mwaka jana, na suluhu kwenye Cecafa 2007.

Tangu wakati huo, ushindi mnono kwa Stars dhidi ya Burundi ni wa mabao 4-1 kwenye mechi ya kirafiki ya kimataifa 1971, wakati yenyewe ikifungwa 2-0.

Burundi kwa mara ya kwanza tangu wakati huo iliifunga Taifa Stars bao 1-0 Agosti 2, 1998 , miaka 27 baadaye kwenye hatua ya kufuzu kwa Mataifa ya Afrika na ikapata matokeo kama hayo kwenye mechi ya marudiano ugenini na kwenye Cecafa Cup, Julai 31, 1999.

Baada ya hapo, ilisubiri kwa miaka 13 mingine hadi kuifunga Stars bao 1-0 Novemba 28, 2012, kwenye Cecafa na 2014 ikaifunga mabao 2-0 kwenye mechi ya kirafiki, wakati Taifa Star ikipapa matokeo ya 2-1, 2-0, 2-1, 3-2, 1-0, 2-0, 1-0, kwenye mechi nyingine za Cecafa na 2-1 kwenye mechi ya kirafiki.

Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije aliitaja Burundi kama moja ya taifa la Afrika linalopiga hatua katika soka kwa sasa.

“Ni taifa ambalo linajaribu kuja juu katika soka, sitarajii kuwa na mchezo rahisi Jumapili,” alisema.