Taifa Stars kutinga Burundi leo mchana

Muktasari:

Mechi ya kwanza ya kuwania kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia, itachezwa kwenye Uwanja wa Stade Intware kesho saa 9.00 alasiri kwa saa za Burundi

Bujumbura, Burundi. Msafara wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' unatarajiwa kuingia nchini Burundi leo saa 6.45 mchana.

Stars inakuja Burundi kwa usafiri wa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Kwa mujibu wa Ofisa wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jonas Kiwia, msafara huo wa Stars uliondoka jijini Dar es Salaam leo saa 4.00 kwa saa za Tanzania.

"Timu yetu inafika na Ndege ya ATCL saa sita na dakika 45 mchana na itafikia kwenye hoteli ya Belair Residence iliyopo hapa jijini Bujumbura," alisema Kiwia.

Msafara huo wa Stars utasimama kwa muda mkoani Kigoma kabla ya kumalizia safari ya kuja Burundi ambako itatua kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Aeroport Melchior Ndadaye.

Ndadaye ni Rais wa kwanza Burundi kuchaguliwa kwa uchaguzi huru lakini alidumu madarakani kwa siku 100 tu baada ya kuuliwa mwaka 1993.