Taifa Stars kupaa Dreamliner’s kesho usiku

Muktasari:

Tanzania inahitaji kushinda katika mchezo huo dhidi ya Cape Verde ili kufufua matumaini yake ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1980 ilipofanya hivyo

Dar es Salaam.Serikali imethibitisha kwamba kikosi cha Taifa Stars kitaondoka kesho usiku ikishindwa kuweka wazi idadi ya waliochangia kwenda kwa safari hiyo.

Mkurugenzi wa Michezo nchini Yusuf Singo amesema kuelekea safari hiyo ya kikosi cha Taifa Stars kwenda Cape verde safari ya timu hiyo ipo palepale kuwa saa tano usiku kesho.

Singo amesema mpaka sasa bado muitikio wa mashabiki wa timu hiyo ni mkubwa kusafiri na timu hiyo.

Aidha Singo amesema bado wahasibu wa wizara na wenzao wa TFF wanaendelea na utaratibu wa kufanyia kazi orodha ya waliofanikiwa kulipia gharama za safari hiyo.

Amesema idadi kamili ya watakaosafiri inaweza kutolewa na waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni, Dk Harrison Mwakyembe atakapoongea mubashara na televisheni ya taifa leo usiku

Naye Kaimu Makamu wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani amesema tayari kikosi cha awali kilichotangulia nchini humo kimeanza kuwapa taarifa juu ya gharama za malazi wakiwa huko.

Nyamlani amesema mtu atakayefanikiwa kusafiri anatakiwa kuwa na kiasi cha dola 40 ya visa ya kuingilia nchini humo huku bei ya hoteli ikiwa ni dola 50.

Amesema TFF bado inajipanga kuhakikisha idadi ya watu watakaoambatana na timu hiyo wanafanikiwa kupata tiketi ya kuingilia uwanjani.