TIMUA VUMBI : Taifa Stars kanyaga twende michuano Chan 2020

Muktasari:

Stars imecheza mechi ya kwanza dhidi ya Kenya katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam japokuwa matokeo hayakuwa mazuri sana, ila yametia moyo kwani bado nafasi ipo ya kujikagua makosa kabla ya mechi ya marudiano huko Kenya, Agosti 4.

TIMU ya taifa ‘Taifa Stars’ iliyoshiriki Fainali za Afcon huko Misri ilitekwa kwa asilimia kubwa na viongozi wa serikali na wanasiasa ambao pia waliibuka dakika za lala salama.

Sio jambo baya, ila waliokuwa wengi sidhani kama walielewa vizuri Taifa Stars iliyokuwa na mchanganyiko wa nyota kibao wanaocheza ndani na nje.

Stars ilishiriki fainali zile baada ya miaka 39 kupita, na Watanzania walikuwa na hamu kubwa japo kutinga tu fainali kitu ambacho kiliwezekana. Iliingia na ikashiriki ingawa ilitolewa kwenye makundi. Binafsi sikuona kama ni jambo baya, bali ni mwanzo mzuri wa kutambua wapi tulipo.

Hivi sasa Stars ambayo ina wachezaji wanaocheza ligi ya ndani inashiriki michuano ya kuwania kufuzu fainali za Chan ambazo zitafanyika mwakani.

Stars imecheza mechi ya kwanza dhidi ya Kenya katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam japokuwa matokeo hayakuwa mazuri sana, ila yametia moyo kwani bado nafasi ipo ya kujikagua makosa kabla ya mechi ya marudiano huko Kenya, Agosti 4.

Ni mechi za mtoano atakayepoteza marudiano basi ataaga mashindano hayo, pengine ndio maana naona wanasiasa wamekaa pembeni hivi sasa, hawahamasishi na huenda hawana uhakika na safari ya Stars huko ugenini.

Lakini cha ajabu, waandishi ambao uwezo wao mkubwa ni kutumia kalamu tu maana uwezo wa kifedha si mkubwa, kwamba watahamasisha Stars kupitia kipato chao kama ilivyo kwa wanasiasa nao waliibuka dakika za lala salama tu. Waandishi wala hawatangazi ahadi za fedha kwa wachezaji wa Stars, wao wamejitoa na kuweka uzalendo mbele na pengine safari yao itakuwa na ugumu kwa kutokuwa na uchumi wa kutosha.

Lakini kwao wanasema iwe njaa, mvua na hakuna kitu kigumu lazima Stars impasue Kenya na kusonga mbele huku wakiongeza nguvu tu ya uhamasishaji na kuwatia moto watu.

Waandishi wameibuka na kujikusanya ili kujitoa kwa ajili ya Stars ambayo haina mastaa pengine kama wale ambao waliwavutia wanasiasa, wameonyesha moyo na nia hata kutojalisha nini kitatokea ugenini kwani wanaamini Stars hii pia inaweza kufanya maajabu na kutinga hatua inayofuata.

Waandishi wamesahau matokeo ya sare tasa pale Taifa wanachokiamini wao ni kushinda ugenini na kusonga mbele huku wakibebwa na kaulimbiu yao ya ‘Tunakanyaga Mpaka Chan’. Hii yote ni kuwatia moyo wachezaji wa timu hiyo wasijione wapweke kwenye safari yao.

Waaandishi watasafiri leo Alhamisi kuelekea Nairobi, Kenya ambapo Stars wenyewe wataondoka kesho Ijumaa na wanahabari hao watasafiri kwa kutumia barabara kwani lengo lao ni kuhakikisha Stars inapata sapoti.

Ni vyema wachezaji wajione fahari na waandishi wa nchi yao kuwa wanawaunga mkono.

Umoja huu wa waandishi wa habari za michezo nchini unatia moja, kwani wamejitoa kwa vitendo kuandika na kwenda moja kwa moja uwanjani, maana hili ni jambo la kitaifa linalostahili kubebwa na kila mmoja.

Wachezaji wa Stars angalieni mioyo ya waandishi hawa isijeruhiwe, warudi na furaha ambayo itawarahisishia safari na kuona kuwa safari ni fupi.

Kwa msingi huu unaoonyeshwa na wanahabari katika kuipigania timu yetu ya taifa, kila Mtanzania anapaswa kujitwisha jukumu kama hilo kwa ajili ya timu yetu, na timu zetu zingine zinazojikuta katika mazingira ya kwenda kupeperusha bendera ya nchi ughaibuni.

Hatuwezi kupiga hatua katika michezo, na kuimarisha furaha iwapo tutaendelea na tabia hii ya kujitokeza katika dakika za majeruhi au hata zile za ushindi ambapo wawakilishi wetu wanakuwa wameshinda kilichowapeleka nje.

Uzalenda kwa ajili ya taifa unaanzia pale ambapo taifa lipo katika mchakato wa mapambano hadi pale linaposhinda.

Hata wale wanaofanikiwa huko duniani wanakuwa na sapoti za watu wao kuanzia katika hatua za awali hadi mwisho, na mfano mzuri ni mzazi kwa mwanaye ambaye bila ya kumjenga vizuri haitarajiwi kwamba atakuja kubadilika na kuonekana kuwa ni raia mwema au atafanikiwa (iwapo ni katika masomo au hata shughuli yoyote anayodhamiria kuifanya).

Uwepo wa dharau katika masuala ya msingi ndilo jambo ambalo limewafanya watu wengi kushindwa kufikia mafanikio, lakini kikubwa zaidi ni kuwa, hata wale waliokuwa wakiwategemea wamewafelisha kwa kutowaunga mkono.

Binafsi bado naamini kwamba timu yetu ya taifa itapenya, lakini kikubwa inahitaji kuungwa mkono ili iweze kufanikiwa. Tunapokwenda Kenya ni lazima tujue kwamba hata wao wamejipanga kuhakikisha kwamba wanaibuka na ushindi, lakini uzalendo wao unaweza kukwaza na mshikamano baina yetu.

Vilevile ipo dhana kwamba, katika kila jambo jema la kitaifa, wananchi tumekuwa tukiitazama zaidi serikali inasema au inafanya nini, badala ya sisi kujiona kwamba tunawajibika moja kwa moja kabla ya serikali. Dhana hii ni mbaya kabisa kufikia malengo tunayojipangia. Ndio maana wapo watu utawakuta wanasubiri hata choo wajengewe na serikali.

Mungu ibariki Taifa Stars, Mungu wabariki waandishi wa habari za michezo. Tunakanyaga mpaka Chan.