TUJIKUMBUSHE: Wambura avuliwa uanachama Simba

TAREHE kama ya leo mwaka 2014, Kamati ya Uchaguzi ya Simba chini ya Mwenyekiti wake Damas Ndumbaro, ilitangaza rasmi kumwengua Michael Wambura kwenye kinyang’anyiro cha nafasi ya Rais.

Wambura alienguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho ambapo alikuwa akigombea sambamba na Evans Aveva pamoja na Andrew Peter Tupa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Juni 29, 2014.

Katika uchaguzi huo nafasi ya Makamu Mwenyekiti iliwaniwa na Geofrey Nyange ‘Kaburu’, Swedy Mkwabi, Jamhuri Kihwelo na Joseph Itang’are ‘Kinesi’ ma kushuhudiwa Aveva na Kaburu wakishinda kwa kishindo.

Ndumbaro ambaye kwa sasa ni Naibu Wizara wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, alitangaza kumwengua Wambura baada ya kubainika kufanya kosa la kufungua kesi Mahakama ya Kisutu kinyume cha Katiba ya Simba.

Ndumbaro alisema kati ya mapigamizi saba aliyowekewa Wambura, mapingamizi matano yalipelekwa Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) wakati mapingamizi mawili ndiyo yalikuwa kesi za msingi walizozijadili.

“Wambura ameondolewa kwa vile kwa sasa si mwanachama halali wa Simba, pia amewekewa pingamizi kwamba aliipeleka Simba mahakamani katika kesi namba 100/2010 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kinyume cha Ibara ya 11(1)(1)(e), (2), 12 (3) na 55 ya Katiba ya Simba mwaka 2010,” alisema Ndumbaro na kuongeza;

“Mwekewa pingamizi alisimamishwa uanachama na Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana Mei 5, 2010 na barua ya Mei 6, 2010 yenye kumbukumbu SSC/MMKT/163/VOL.40/11 na hivyo basi anapoteza sifa na haki ya kuwa mwanachama wa Simba.”

“Mwekewa pingamizi amekiuka Katiba ya Simba, TFF na FIFA kwa kuipeleka Simba mahakamani katika kesi namba 100/2010, pia alianza kampeni kabla ya muda wa kampeni na alikiuka Katiba ya Simba kwa kukubali uteuzi batili kuwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji, pia hana maadili ya uongozi kwasababu alikiuka maadili akiwa kiongozi wa FAT sasa TFF na si mwabijikaji,” alifafanua Ndumbaro.

Ndumbaro ambaye ni Wakili alisema Kamati yake ilitumia kujadili na kutolea uamuzi suala la kuifungulia kesi namba 100/2010 aliofungua Wambura kinyume na ibara ya 11(1)e (2), 12 (3) na 55 ya Katiba ya Simba ya mwaka 2010.

Wambura ambaye alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa TFF kwenye uongozi wa sasa wa shirikisho hilo, alijikuta aking’olewa na kufunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi na ukatatishaji wa fedha kabla ya kuachiwa baada ya kukubali kulipa Sh 100 milioni ili awe huru.