TUJIKUMBUSHE : Ngoma, Tambwe wainyoosha Kagera Sugar

Muktasari:

Kwa wanaokumbuka mchezo huo, wageni Kagera ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya tisa tu baada ya Mbaraka Yusuf kuunganisha kwa kichwa krosi ya Salum Kanoni kabla ya Donald Ngoma kuisawazishia bao dakika ya 25 akimalizia majalo muru ya Juma Abdul.

INAWEZEKANA Kocha Luc Eymael wa Yanga bado anaikumbuka vizuri Kagera Sugar kwani ndio waliomkaribisha kwa aibu nchini pale walipowafumua mabao 3-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Januari 15 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Lakini buana, katika kumbukumbu zilizopo tarehe kama ya leo, yaani Aprili 3, lakini mwaka 2016 Kagera haohao walichezea mvua kwa Yanga kwenye uwanja huo huo wakati huo Yanga ikiwa chini ya Babu, Hans Pluijm.

Katika mechi hiyo ambayo ni moja ya ilizoipa Yanga ushindi na kwenda kutwaa ubingwa kwa rekodi ya aina yake ya kuvuna alama 73 na mabao 70 katika mechi 30 tu, vijana wa Jangwani walishinda mabao 3-1.

Kwa wanaokumbuka mchezo huo, wageni Kagera ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao dakika ya tisa tu baada ya Mbaraka Yusuf kuunganisha kwa kichwa krosi ya Salum Kanoni kabla ya Donald Ngoma kuisawazishia bao dakika ya 25 akimalizia majalo muru ya Juma Abdul.

Dakika 34, Yanga walipata penalti baada ya Shaaban Ibrahim ‘Chogo’ kumkwatua Ngoma na Kelvin Yondani alipiga shuti lililodakwa na kipa wa Kagera, Andrew Ntara.

Kipindi cha pili kilianza kwa Kagera kupata pigo baada ya Chogo kulimwa kadi ya njano ya pili iliyozaa nyekundu sekunde chache baada ya kuanza kwa kipindi hicho na Yanga kuitumia vyema kuwanyoosha Wana Nkurukumbi kwani dakika ya 62 waliandika bao la pili.

Bao hilo liliwekwa kimiani na aliyekuja kuwa Mfungaji Bora wa msimu huo, Amissi Tambwe aliyewahadaa mabeki wa Kagera kabla ya kumtungua kipa Ntara. Tambwe alimaliza msimu akiwa na mabao 21 na kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kufunga idadi kubwa ya mabao, ambayo hata hivyo ilikuja kuvunjwa msimu uliopita na Meddie Kagere wa Simba aliyefunga mabao 23. Kagera walikuja kunyong’onyeshwa ‘jioni’ pale beki wa kushoto, Haji Mwinyi alipokwamisha bao la tatu kwa kichwa akimalizia kona tamu ya winga, Simon Msuva dakika ya 89.