TTF kuendesha semina ya Taekwondo

Muktasari:

  • Akizungumzia mafunzo hayo mratibu, David Samson ambae ni mmoja wa wakufunzi katika semina hiyo, alisema mafunzo yatafanyikia Arusha katika viwanja vya AICC kuanzia Janury 20 hadi 27 ambapo washiriki watatakiwa kuthibitisha ushiriki wao mapema kwa ajili ya maandalizi ya ukumbi na ambapo watakaotoka mikoani watajigharamia chakula na malazi.

ARUSHA.Shirikisho la mchezo wa Taekwondo nchini (TTF) kwa kushirikiana na wakufunzi wa ndani na nje ya nchi linatarajia kutoa semina ya wazi ya wiki moja juu ya sheria mpya za upangaji wa pointi za uwanjani zilizotolewa hivi karibuni na shirikisho la mchezo huo kimataifa (ITF) na shirikisho hilo duniani (WTF).

Sheria hizo zilizotolewa hivi karibuni zilisambazwa na Shirikisho la Taekwondo duniani (WTF) kwa kushirikiana na shirikisho la mchezo huo kimataifa (ITF) kwa semina ya mwezi mzima kwa wakufunzi wa kimataifa kutoka nchi zaidi ya 50 duniani zinazoshiriki mchezo huo na mashindano mbali mbali.

Mafunzo hayo yaliyofanyika Makao Makuu ya mchezo wa Taekwondo duniani (Korea kusini) kwenye Mji wa Muju mwezi Novemba 2018, kwa Tanzania wakufunzi wawili waliwakilisha ambao ni David Samson na Partick Majaliwa wenye mafunzo ya ngazi ya juu ya mkanda mweusi (Black Bell) na shahada (degree) tano za Taekwondo.

Akizungumzia mafunzo hayo mratibu, David Samson ambae ni mmoja wa wakufunzi katika semina hiyo, alisema mafunzo yatafanyikia Arusha katika viwanja vya AICC kuanzia Janury 20 hadi 27 ambapo washiriki watatakiwa kuthibitisha ushiriki wao mapema kwa ajili ya maandalizi ya ukumbi na ambapo watakaotoka mikoani watajigharamia chakula na malazi.

“Tutakuwa na wageni wa mchezo huu kutoka Ethiopia na Korea ambao tutasaidiana nao kuwaelimisha wachezaji wetu juu mabadiliko ya pointi za mapigano na sheria za ulingoni kabla ya kalenda ya mashindano haijatoka ili kuanza kufanyia mazoezi”

Alisema baadhi ya sheria za mchezo wa Taekwondo ambazo zimebadilishwa ni muda wa wanafunzi kupanda ngazi ya mkanda wa kijani na njano ambayo ilikuwa miezi mitatu sasa ni minne, lakini pia sheria za ulingoni za kuvuna pointi sambamba na aina mpya ya upiganaji (Pumse) ambayo yanaandaliwa mashindano yake na ITF.

“Semina hii watu waliothibitisha hadi sasa kushiriki ni zaidi ya 40 kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro bado hatujapokea washiriki kutoka mikoa mingine lakini nafasi bado zipo maana mafunzo ni bure na tunatoa mafunzo haya mapema maana sheria hizi zitaanza kutumika mwaka huu kwenye mashindano mbali mbali ya ndani na nje ya nchi.”