TTB yampa Samatta ubalozi wa Utalii Tanzania

Thursday July 11 2019

 

By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta ametangazwa rasmi kuwa balozi wa kujitolea wa utalii na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Samatta mshambuliaji wa timu ya KRC Genk ya Ubelgiji ameingia makubaliano hayo leo Julai 11, 2019 na kusaini mkataba na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Akizungumza baada kusaini makubaliano hayo Samatta amesema ni heshima kwake kutambulika rasmi kama balozi wa utalii wa nchi yake kwa kuwa ni kitu ambacho amekuwa akikifanya kwa muda mrefu.

Samatta alisema anajivunia kutangaza utalii wa ni matumaini yake ubalozi wake utasaidia kuwahamisha watu kutoka mataifa mbalimbali kuja nchini.

“Ni fahari kubwa kwangu kuwa balozi wa kujitolea, naifanya kazi hii bure kabisa kwa ajili ya nchi yangu na ikizingatiwa ni kitu ambacho ninakipenda na nimekuwa nikikifanya siku zote.”

“Kwa kuwa kuna watu wengi wanaonifuatilia na wanajua kwamba mimi ni Mtanzania basi watapata fursa ya kuona Tanzania kuna nini na wakivutiwa watakuja kutembelea,” alisema Samatta

Advertisement

Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB, Devota Mdachi alisema watamtembeza Samatta kwenye vivutio mbalimbali vilivyopo nchini ili avifahamu na kuweza kuvitangaza.

Katika makubaliano hayo Samatta atatumia mitandao yake ya kijamii kutangaza vivutio vya utalii pia atatumika kwenye matangazo ya kuhamasisha utalii.

Advertisement