TP Lindanda kazi ndio imeanza FDL

Muktasari:

Pamba itacheza mechi tatu mfululizo katika uwanja wa nyumbani (Nyamagana)ikianza dhidi ya Mashujaa Oktoba 20,Mgambo Shooting Oktoba 27 kisha Polisi Tanzania Novemba 2 mwaka huu.

MWANZA. MITAMBO imewaka unaambiwa, baada ya ushindi wa mabao 3-1 walioupata Pamba dhidi ya Trans Camp kwenye Ligi Daraja la Kwanza Kocha wa timu hiyo Juma Yusuph ‘Sumbu’ amepandwa na ‘mzuka’ na kutamba kuwa kazi ndio imeanza.

Timu hiyo kongwe ya Jijini Mwanza ilianzia mechi zake ugenini,ambapo awali ilikung’utwa bao 1-0 dhidi ya Dodoma ambapo juzi iliweza kuwachezesha kwata Trans Camp kwa kuwalaza mabao 3-1.

Kocha Sumbu alisema kuwa licha ya kuambulia pointi tatu badala ya sita katika mechi za ugenini lakini amekoshwa na kiwango walichoonyesha vijana wake na kwamba kazi ndio imeanza.

Alisema kuwa kwa sasa wanarudi nyumbani nyumbani kuhakikisha mechi tatu watakazocheza katika uwanja wa Nyamagana hawaachi kitu ili kuweza kufikia malengo yao waliyojiwekea.

“Kwanza niwapongeze vijana kwa kazi nzuri waliyoifanya,lakini niseme kuwa bado ndio safari imeanza tunahitaji mechi tatu tutakazocheza nyumbani kuhakikisha tunashinda zote”alisema Sumbu.

Kocha huyo aliongeza kuwa kipindi hiki ni wadau na wapenzi wa timu hiyo kutoa ushirikiano ili kuweza kufikia malengo ya kuhakikisha msimu ujao Pamba inashiriki Ligi Kuu.

Alisema kuwa licha ya ugumu wa Ligi uliopo kwa timu zote kuhitaji nafasi ya kucheza Ligi Kuu lakini Benchi la Ufundi limejipanga vyema kupambana na mikiki mikiki hiyo.

“Huu ni muda wa kila mdau wa Soka Jijini Mwanza pamoja na mashabiki wa timu yetu kutoa ushirikiano kuisaidia Pamba kuhakikisha tunaungana na kuipandisha Ligi Kuu”alisema Kocha huyo.