TORREIRA:Jibu la kiungo cha Arsenal tangu Patrick Vieira

Saturday December 8 2018

 

LONDON, ENGLAND

KATIKA mechi tatu kati ya nne zilizopita za Arsenal, kiungo Lucas Torreira amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi. Ameingia katika Ligi Kuu ya England na kasi ya ajabu. Na sasa Torreira ametibu tatizo sugu la eneo la kiungo la Arsenal ambalo lilikosa ugumu kwa kipindi kirefu tangu kuondoka kwa Patrick Vieira. Ni nani huyu Lucas Torreira?

 

Mtoto halisi wa Uruguay

Jina lake kamili ni Lucas Sebastián Torreira Di Pascua. Alizaliwa Februari 11, 1996 katika mji wa Fray Bentos nchini kwao Uruguay. Alianza kucheza soka katika klabu ya eneo lao ya  I.A. 18 de Julio ya Fray Bentos. Mwaka 2013, alijiunga na timu ya  vijana ya Montevideo Wanderers.

Kutokana na kiwango alichoonyesha akiwa kijana, licha ya umbo lake dogo lakini klabu mbalimbali zilianza kuvutiwa na uwezo wake wa kujituma. Hatimaye klabu ya Pescara ilifanikiwa kumnasa na kumpeleka katika timu yao ya vijana.

 

Atoka kwao, atua Pescra ya Italia

Torreira alitua klabuni hapo kama mchezaji wa timu ya vijana. Hata hivyo kabla ya kuanza kwa simu wa 2014-15 aliitwa katika kikosi cha kwanza na mnamo Oktoba 25, 2014 kwa mara ya kwanza alikaa katika benchi la kikosi cha kwanza.

Alicheza mechi yake ya kwanza Ligi daraja la kwanza Italia maarufu kama Serie B katika pambano dhidi ya Varese mnamo Mei 16, 2015 akianza katika pambano hilo. Hata hivyo alitolewa katika dakika ya 58 na nafasi yake kuchukuliwa na Matteo Politano.

Alicheza mechi tano ikiwemo mechi za mtoano katika tiketi ya kusaka kupanda Ligi Kuu. Kiwango chake kilianza kuzivutia klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Italia lakini ilikuwa ni timu ya Sampdoria ndio ambayo ilionyesha nia zaidi ya kumtwaa.

 

Sampdoria yamnasa, yamuacha kwa mkopo

Julai Mosi, 2015, Torreira alinaswa na klabu ya Ligi Kuu ya Italia Sampdoria kwa dau la Euro 1.5 milioni, lakini hata hivyo klabu hiyo iliamua kumuacha katika klabu ya Pescara kwa ajili ya kuhakikisha anaendelea kupata uzoefu.

Alipelekwa kwa mkopo katika siku ya pili mnamo Julai 2, 2015. Alianza kuonyesha makali yake mnamo Agosti 9, 2015 akifunga bao lake la kwanza la soka la kulipwa katika pambano dhidi ya FC  Südtirol michuano ya Coppa Italia.

Kwa ujumla alicheza mechi 26 na kufunga mabao matatu. Vile vile alicheza mechi tatu na kufunga bao moja katika mechi mtoano kwa ajili ya kutafuta mbabe ambaye angepanda daraja na kwenda Ligi Kuu Serie A.

 

Arudi Sampdoria, atamba

Baada ya kipindi chake cha mkopo kwa Pescara kumalizika, Torreira alirudi katika klabu yake mama ya Sampdoria mnamo Julai Mosi, 2016. Alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Italia mnamo Agosti 21, 2016 katika pambano la ufunguzi dhidi ya Empoli.

Katika pambano hilo, Torreira alicheza dakika zote 90. Alionyesha kiwango kikubwa na kuanzia hapo alianza kuwa mchezaji muhimu katika kikosi hicho na kutamba msimu mzima wa 2016/17.

Katika msimu uliofuata ambao ni wa 2017/18, Torreira alizidi kuonyesha umuhimu wake kikosini hapo huku akifanya kazi ngumu ya kukaba, kupiga pasi za mwisho na kufunga. Alifunga mabao muhimu ikiwemo bao la pili la Sampdoria katika ushindi muhimu wa mabao 3-2 dhidi ya mabingwa watetezi, Juventus.

 

Atua Arsenal

Torreira alitua rasmi Arsenal Julai 10, 2018 kwa dau la pauni 26 milioni huku akipewa jezi namba 11 ambayo awali ilikuwa inavaliwa na kiungo, Mesut Ozil ambaye alipewa jezi namba 10 baada ya Jack Wilshere kuondoka.

Torreira alicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu mnamo Agosti 12 akiingia dakika ya 70 katika kichapo cha 2-0 kutoka kwa Man City nyumbani. Alitengeneza bao lake la kwanza katika pambano dhidi ya Cardiff City akipika bao la Alexandre Lacazette katika ushindi wa mabao 3-2 ugenini.

Alicheza mechi yake ya kwanza kamili kwa Arsenal katika pambano la Europa dhidi ya FC Vorskla Poltava waliloshinda 4-2. Alitolewa katika dakika ya 57 na nafasi yake kuchukuliwa na Mattéo Guendouzi. Kiwango alichoonyesha katika sare ya 1-1 dhidi ya Liverpool kilisababisha wachambuzi na mashabiki wengi kumsifu.

Wikiendi iliyopita alifunga bao lake la kwanza kwa Arsenal akipokea pasi nzuri kutoka kwa Pierre-Emerick Aubameyang kabla ya kumchambua vema kipa wa Tottenham, Hugo Lloris na kufunga bao la nne katika ushindi wa mabao 4-2 wa Arsenal dhidi ya wapinzani wao.

 

Atesa na jezi ya Uruguay Russia

Baada ya kuzichezea timu za vijana za Uruguay kwa nyakati tofauti, Torreira ambaye ana asili ya Hispania na anamiliki Pasipoti ya Hispania aliitwa katika kikosi cha wakubwa cha Uruguay kwa mara ya kwanza Machi mwaka huu kwa ajili ya michuano ya China Cup. Alicheza mechi yake ya kwanza katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Czech.

Mei mwaka huu aliitwa katika kikosi cha awali cha wachezaji 26 cha Uruguay kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya kombe la dunia nchini Russia. Hata hivyo alifanikiwa kupenya katika orodha ya wachezaji 23 wa mwisho ambao wangekwenda Russia.

Katika pambano la kwanza dhidi ya Misri alitokea katika benchi lakini akaanza katika mechi zilizofuata dhidi ya Saudi Arabia na kisha wenyeji Russia. Alianza pia katika katika pambano la mtoano dhidi ya Ureno ambalo walishinda mabao 2-1 yote yakifungwa na Edinson Cavani.

 

USIPIME

-DAVID de Gea ndiye kipa wa kwanza msimu huu kuucheza mpira uliolenga lango uliopigwa na Pierre-Emerick Aubameyang.

-ANTHONY  Martial ni mchezaji wa pili wa Manchester United kufunga bao katika siku ya kusheherekea kuzaliwa kwake. Wa kwanza ni Wayne Rooney aliyefunga mechi dhidi ya Arsenal Oktoba 2004.

-RYAN Fraser wa Bournemouth ndiye mchezaji aliyepika mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu ya England mpaka sasa. Mabao saba.

-Neil Warnock wa Cardiff City ni kocha wa  nne katika Ligi Kuu ya England kufundisha akiwa na umri wa miaka 70 au zaidi. Wengine ni Sir Bobby Robson, Sir Alex Ferguson na Roy Hodgson

 

 

Advertisement