TIMUA VUMBI : Simba ya nini kugombea fito ujenzi nyumba moja!

Muktasari:

Mo Dewji ana nguvu upande wa uwekezaji na Mkwabi pia ana nguvu upande wa klabu kwani ndiye anasimamia mali za klabu ya Simba tangu wanachama walipomwamini na kumchagua Novemba mwaka jana.

Ndani ya Simba hakuko sawa, watuwalianza kusigana chini kwa chini, kila mmoja akitaka kulinda masilahi yake na sasa mambo yako hadharani, hamna kificho tena.

Tajiri na mwekezaji ndani ya Simba, Mohamed ‘Mo’ Dewji na Mwenyekiti wa klabu, Swedy Mkwabi, imedaiwa hawapatani, wanasigana, wanabishana, wanashindwa kufikia makubaliano.

Mabishano hayo yameonekana kumkera wazi wazi Mo Dewji ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, ambaye alianza kuandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii maneno ya mafumbo ingawa hakuweka wazi nini tatizo.

Inawezekana alikuwa akiandika kwa kujifurahisha, lakini moja kwa moja ilitafsiriwa kuwa analenga fukuto lililopo ndani ya Simba baina yake na Mkwabi.

Mo Dewji ana nguvu upande wa uwekezaji na Mkwabi pia ana nguvu upande wa klabu kwani ndiye anasimamia mali za klabu ya Simba tangu wanachama walipomwamini na kumchagua Novemba mwaka jana.

Kwa vile kila mmoja ana masilahi upande wake, ni lazima kila hoja inayowasilishwa isikilizwe, ijadiliwe na ikubalike pande zote mbili pasipo kumwathiri yeyote.

Katika maandiko mbalimbali yaliyokuwa yakichapishwa na vyombo vya habari hasa magazeti na mitandao ya kijamii ilionyeshs kwamba Mo Dewji kuna mambo anahitaji yafanywe kwa uharaka ndani ya Simba lakini Mkwabi amekuwa akiyakwamisha ndio maana tajiri hiyo anaona kama anamhujumu.

Huenda ni kweli ama si kweli kwamba Mo Dewji anahujumiwa na Mkwabi kwani kati ya hao wawili hakuna aliyejitokeza hadharani kuelezea ukweli hata kama habari zinaandikwa kutoka kwenye vyanzo vya ndani ya Simba.

Sidhani kama haya yanaoendelea ndani ya Simba yanaleta afya kwa Simba ambayo imefanya vizuri zaidi kwa misimu miwili ya ligi sana sana yatawarudisha nyuma na kuanza kujuta.

Mo Dewji alikuwa anadaiwa kujiondoa Simba, sawa, huenda uamuzi wake ukawa sahihi lakini ikielezwa kwamba hata Sh 5bilioni zake ambazo amekuwa akitoa kwa kuikopesha Simba atasamehe, hilo nalo ni jambo la kiungwana lakini je kitu gani kimeshindikana kukaa pamoja na kujadili ikiwa ni pamoja na kuziondoa tofauti zenu maisha yaendelee?

Mo Dewji ambaye ana asilimia 49 za uwekezaji ndani ya Simba huenda pia anatumia hasira zaidi na kutaka kutoa maamuzi ambayo yatawagharimu wengi ndani ya klabu hiyo.

Simba ina muongozo wake ambao wanapaswa kuufuata hivyo viongozi wote hawana budi kufuata mwongozo unasemaje na asiwepo yeyote ambaye anakuwa juu ya mamlaka ya Simba.

Kuna jambo ambalo pia lilidaiwa kwamba uitishwe mkutano wa dharura ili kama vipi Mkwabi ajiuzulu, sioni kama kuna haja hiyo kwani hakuna lisilozungumzwa na kumalizwa ingawa pia Mkwabi anaweza kuwa na uamuzi wake kama ni kujiuzuku ama kuendelea kupigana vita ndani ya Simba.

Naamini kwamba kila mmoja katika msuguano huu ana nia nzuri ya kuijenga Simba.

Sitaki kuamini kwamba kuna mmoja kati yao anataka kuona Simba inakuwa timu nyanya kwenye Ligi Kuu ya Bara na inanyanyasika kwa vipigo vikubwa vikubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambako itashiriki tena msimu ujao.

Ni nani kati ya wanaovutana anayeweza kusema kwamba hana ndoto ya kuona Simba inafikia levo za klabu kubwa za Afrika?

Ni nani kati ya wanaosigana hapendi kuona siku moja Simba inacheza mechi zake zote kubwa za nyumbani kwenye uwanja wake wa nyumbani?

Je, yupo ambaye hatamani kuona Simba inakuwa na kituo chake kikubwa cha michezo sambamba na akademi kubwa inayouza wachezaji hadi Ulaya?

Ukijiuliza maswali yote hayo, unaona ni wazi kwamba hakuna kati yao ambaye hatamani kuona Simba inatawala soka la Afrika ikilileta katika ardhi ya Tanzania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mara kwa mara.

Hizo zote ni ndoto za kila mwana Simba.

Sasa kama nia ya kila mmoja ni kujenga nyumba moja ya Simba, ni kwa vipi kunakuwa na vita katika kugombea fito za kujengea?

Mafanikio ambayo Simba iliyapata msimu uliopita ni ya kujivunia na ni wakati muafaka kwa kila mwanaSimba kuweka nguvu katika kuhakikisha timu inafika mbali zaidi ya robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kama kila mmoja aliafiki kwamba uwekezaji ni njia sahihi ya kuiondoa Simba kutoka katika mfumo wa kizamani ambao uliifanya ikadumaa kwa zaidi ya miaka 80 tangu ilipoanzishwa, basi ni vyema kila mmoja kwa nafasi yake akatumia kila juhudi kuhakikisha mwafaka unapatikana kati ya pande zinazovutana kuhakikisha klabu inatumia muda mwingi uliopo sasa kutengeneza maendeleo kuliko kutumia muda mwingi katika kuvutana nyuma.

Wahusika katika mgogoro wasitazamane kama paka na panya, bali watazamane kama wanajeshi wanaopeana ishara kwa kusonga mbele katika kupigania kile kilicho chao.

Kila jambo lina ufumbuzi. Pande zinazosigana zinapaswa kutambua kwamba zipo kwa ajili ya kuijenga Simba moja.

Kama kila mmoja anajivunia kuwa mwanaSimba, ina maana kwamba kila mmoja anajisikia fahari kuipigania klabu hiyo akifahamu mafanikio ya Simba ni mafanikio ya kila mmoja na yatamfanya kila mmoja kujivunia juhudi zake katika kuijenga klabu.