TIMUA VUMBI : Nimemwelewa Amunike kuhusu nidhamu, tusimbeze

Muktasari:

Mbwana Samatta, Simon Msuva, Hassan Kessy, Thomas Ulimwengu na wengineo akiwemo Adi Yusuf anayekipiga soka la England katika klabu ya Blackpool, ni miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha Stars ambao kwa nafasi zao wanabeba matumaini ya Watanzania ya kufanya vyema.

KIKOSI cha timu ya Taifa, Taifa Stars kimeshatajwa na wengi wameshayajua majina ya nyota watakaoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afcon inayotarajia kuanza baadaye mwezi huu huko Misri.

Ni michuano ambayo kwa nchi yetu kufuzu ni mara ya pili tangu mwaka 1980 ikiwa ni miaka 39 mpaka sasa.

Ni miaka mingi na hakika kila Mtanzania aliyejaaliwa kuona fursa hii ya Taifa letu, ni wazi anafuraha moyoni kutokana na mara kwa mara Watanzania waliishia kugawana timu za kushabikia pale inapofikia mashindano haya makubwa.

Tumekosa bahati hiyo kutokana na sababu nyingi lakini kubwa ikiwa ni kukosa wachezaji wenye viwango tofauti na mataifa ya wenzetu. Maandalizi pia ni moja ya sababu ya kushndwa kufuzu mara zote hizo kwa miaka hiyo 39.

Hata hivyo, kwa kipindi cha karibuni mambo yamebadilika na Watanzania wameanza kushuhudia timu yao ya Taifa ikianza kuwa imara hasa kutokana na kuwepo kwa wachezaji wengi wanaosakata soka nje ya mipaka ya Tanzania na nje ya Afrika.

Mbwana Samatta, Simon Msuva, Hassan Kessy, Thomas Ulimwengu na wengineo akiwemo Adi Yusuf anayekipiga soka la England katika klabu ya Blackpool, ni miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha Stars ambao kwa nafasi zao wanabeba matumaini ya Watanzania ya kufanya vyema.

Kocha wa Stars Emanuel Amunike ametaja kikosi hiko na kuacha baadhi ya nyota wengine kutokana na sababu mbalimbali kubwa na ambayo imekuwa ikiongelewa sana na baadhi ya makocha sio tu wa timu za taifa, bali klabu ni kuhusu nidhamu.

Suala la nidhamu kwa wachezaji limekuwa ishu kubwa na haliwezi kuvumilika kwa makocha.

Wachezaji wengi wamekuwa na nidhamu ndogo kiasi cha kuwakera hata makocha wao na kusababisha kuwekwa benchi.

Wakati mwingine makocha wamekuwa wakivumilia matusi na maneno kutoka kwa wadau na mashabiki wa soka pale anapomwacha mchezaji kwenye kikosi cha kwanza, bila mashabiki hao kujua kosa la mchezaji.

Hata pale kocha anapoweka wazi sababu ni utovu wa nidhamu, kutokana na kiwango cha mchezaji husika, mashabiki wanaona kaonewa na labda anatofauti na kocha.

Tumeona mashabiki wengi wa soka baada ya uteuzi wa kikosi cha Stars wakimlaumu Kocha Amunike kwa sababu ya kuwaacha nje wachezaji Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude ambao kila mtu anaamini katika uwezo wao wa soka.

Ndio wana viwango na walistahili kuwepo katika kikosi cha timu ya taifa, lakini tusisahau kwamba kwenye kila jambo au kazi yoyote ile nidhamu ni muhimu kwa wafanyakazi.

Hata wachezaji nao ni wafanyakazi kama wafanyakazi wengine wa ofisini na wanalipwa kutokana na kazi wanayofanya kama wengine wa ofisini wanavyolipwa.

Nidhamu nayo inahitajika kwenye soka na ndio maana Kocha Amunike alilizingatia hilo baada ya kuona wachezaji hao wameshindwa kufikia sifa za wachezaji aliowataka katika kikosi chake.

Mchezaji anaitwa kikosini kwaajili ya kambi anakataa au anachelewa, huo ni utovu wa nidhamu na kamwe sio u kwa timu ya taifa, hata klabu zinatakiwa zichukulie maanani kuwaadhibu wachezaji wenye tabia hizo ili kuufanya mchezo wa soka uwe na maana kwa sasa na kwa vizazi vijavyo.

Ni wazi kwa kilichotokea kwa Ajibu na Mkude itakuwa fundisho kwa wanasoka wengine wanaotamani kuvaa uzi wa Stars, moja kati ya sifa kubwa kwa wanasoka kabla ya kusataafu.

Suala la nidhamu lisifumbiwe macho hata kwa makocha wa klabu na wachezaji wajifunze nini nidhamu hasa wawapo kambini na sio kujiona wameshakuwa mastaa na wanaweza kufanya lolote wakiamini kutokana na viwango vyao, hawataweza kuguswa.

Tusimlaumu Amunike kwa alichokifanya na sasa ni wakati wa kuiunga mkono timu yetu ya taifa iweze kufanya vyema kwenye michuano hiyo ya Afcon huko Misri,.