Thomas Ulimwengu: Mpambanaji mwenye historia ya kuvutia Afrika

Muktasari:

Ulimwengu aliachana na AFC Eskilstuna kutokana na kusumbuliwa kwake na majeraha hivyo, aliamua kujitibia mwenyewe kwa kufanyiwa oparesheni ya goti ambalo lilikuwa likimsumbua mjini Cape Town, Afrika Kusini.

YAANI huyu Thomas Ulimwengu hana tofauti kabisa na aliyekuwa mshambuliaji wa zamani wa Manchester United, Mfaransa Louis Saha. Usipime kabaisa kwani, nyota hawa kwa nyakati tofauti walizichezea klabu nne ndani ya miaka minne.
Baada ya kuvunja mkataba wake kwenye klabu ya Al-Hilal ya Sudan, wadau wengi wa soka walikuwa wakisubiri ni wapi ambapo Ulimwengu atatua huku wengine wakimhusisha na kurudi klabu za nyumban.
Lakini, wiki chache jamaa akaibukia zake Algeria na kujiunga na wapinzani wa Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, JS Saoura.
Tangu Ulimwengu aondoke TP Mazembe kwa lengo la kutaka kupiga hatua kama ilivyokuwa kwa Mtanzania mwenzake, Mbwana Samatta haikuwa vile alivyopanga licha ya kuendelea kupambana.
Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011 alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza.
Ulimwengu na Samatta wamecheza wote Mazembe ya DR Congo na kushinda mataji kadhaa pamoja kwenye klabu hiyo ya tajiri, Moses Katumbi, ambaye aliwahi kuwa Gavana wa Katanga, eneo la Kusini mwa nchi hiyo.
Samatta alikuwa wa kwanza kuondoka Mazembe, Januari 29, 2016 na kutimkia zake KRC Genk ya Ubelgiji, kisha Ulimwengu akafuata Julai Mosi, 2017 kwa kutimkia zake Sweden kwa mara nyingine tena kwenye klabu ya AFC Eskilstuna.
Katumbi alijitihida kupitia nguvu zake kifedha kuwabakisha kwa vipindi tofauti washambuliaji hao wa Kitanzani hasa Samatta, lakini ilishindikana waliamini kuwa muda umefika wa kwenda kukabiliana na changamoto mpya za soka barani Ulaya.
Muda ulipofika Ulimwengu naye akaondoka tena akiwa mchezaji huru maana alisubiri mkataba wake umalizike.
Kibaya kwa Ulimwengu hakuondoka moja kwa moja kwenda kujiunga na AFC Eskilstuna ya Sweden, alikaa bila ya kuwa na timu kwa miezi kadhaa ndipo alipoibukia kwenye klabu hiyo, mwanzoni mwa mwaka jana.
Alipata muda wa kufanya mazoezi na kikosi cha kwanza na hata kwenda kwenye maandalizi ya msimu mpya kipindi hicho nchini Hispania ambako AFC Eskilstuna waliweka kambi na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki.
Ulimwengu aliachana na AFC Eskilstuna kutokana na kusumbuliwa kwake na majeraha hivyo, aliamua kujitibia mwenyewe kwa kufanyiwa oparesheni ya goti ambalo lilikuwa likimsumbua mjini Cape Town, Afrika Kusini.
Alifanya mazoezi ya kujiweka fiti chini ya walimu tofauti ili kurejesha kiwango chake kwa haraka na kuanza tena kusaka klabu za kuzichezea huku akitembea nchi kadhaa ikiwemo Italia.
Alivyorejea tu kwenye hali yake, Machi mwaka jana akaibukia Bosnia ambako alifanya majaribio na kufuzu klabu ya Sloboda Tuzla na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki.
Inshu za vibali vya kazi nchini humo ndiyo iliyomkwamisha kucheza Ligi Kuu Bosnia na  Herzegovina ndipo Wasudani, Al Hilal  walipotumia mwanya huo, Mei 22 kumnasa kwa mkataba wa miezi sita.
Mshambuliaji huyo wa Kitanzania aliiongoza Al Hilal kwenye mchujo ‘Play Off’ kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Sudan mwaka jana na kucheza michezo Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya kuvunja mkataba na kujiunga na JS Saoura.
Katika mahojiano yake ya kwanza baada ya kutua kwa Waarabu hao, Ulimwengu anasema mapango wake ni kuisaidia klabu hiyo kufikia malengo kwa kipindi chote atakachoichezea.
“Nitajitahidi kuisaidia timu yangu kufunga mabao kila itavyowezekana ili tuweze kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, kikubwa ni wachezaji wenzangu kunipa ushirikiano wa kutosha,” anasema mshambuliaji huyo.
Huyo ndiye Ulimwengu, upande wa Saha ambaye alistaafu Agosti 8, 2013, alizichezea Everton, Tottenham, Sunderland za England na Lazio ya Italia ndani ya miaka minne toka 2009 hadi 2013.

WASIFU WAKE
Jina Kamili: Thomas Emmanuel Ulimwengu
Kuzaliwa: Juni 14, 1993
Mahali: Tanga, Tanzania
Urefu: 1.78 m (5 ft 10 in)
Timu: JS Saoura
Nafasi: Mshambuliaji