TFF yatia mkono uchaguzi Yanga

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF, Ally Mchungahela

Muktasari:

  • Akizungumza na gazeti hili, Mchungahela alisema wanachama wote wenye kadi hai za zamani au mpya wanaruhusiwa kupiga kura kuchagua mgombea wanayemtaka.

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema kadi za zamani ruksa kutumika katika uchaguzi wa Yanga uliopangwa kufanyika Januari 13, mwaka huu.

Ufafanuzi huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF, Ally Mchungahela muda mfupi kabla ya kuanza kampeni za uchaguzi.

Akizungumza na gazeti hili, Mchungahela alisema wanachama wote wenye kadi hai za zamani au mpya wanaruhusiwa kupiga kura kuchagua mgombea wanayemtaka. “Iwe kadi ya kitabu au mpya wote wana haki ya kupiga kura jambo hili linabidi liwe wazi. Kadi ziwe hai wanachama wana haki ya kumchagua mgombea yeyote wanayemtaka,” alisema Mchungahela. Pia alisema wagombea wana haki ya kufanya kampeni kuanzia leo hadi Januari 12, katika kila tawi ambalo wanataka kunadi sera zao.

“Kila sehemu mgombea ana haki ya kufanya kampeni, tawi ni mali ya klabu na siyo mtu, hivyo kama kutakuwa na mtu hataki kusikia kampeni ni bora aondoke eneo hilo lakini amuache mgombea afanye kazi yake,” alisema mwenyekiti huyo.

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Siza Lyimo, aliwataka wanachama kulipia kadi zao ili kuwa na sifa ya kupiga kura na kuchagua mgombea wanayemtaka katika uchaguzi huo. Uchaguzi utafanyika Ukumbi wa Polisi Oysterbay, jijini.