TFF yatambulisha jezi mpya ya Taifa Stars

Wednesday June 12 2019

 

By Thobias Sebastian

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kamati saidia Taifa Stars ishinde na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia wametambulisha jezi mpya za Taifa Stars kwa ajili ya Afcon2019, Misri.

Jezi hiyo mpya ya Taifa Stars imepambwa kwa picha ya Twiga ubavuni pamoja na michilizi ya rangi nyeusi na bluu bahari kifuani.

Halfa hilo imefanyika leo Jumatano mchana katika hoteli ya Serena, akizungumza katika halfa hiyo Karia alisema wanatambulisha jezi aina mbili yanyumbani na ile ya ugenini.

"Jezi hizi za njano zitatumika katika mechi za ugenini na zitanza kutumika katika mechi ya kesho ya kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Misri," alisema Karia.

"Hizi zenye rangi ya bluu zitatumika katika mechi zote tutakazocheza nyumbani.

"Tumempa Makonda jezi hii ya nyumbani na nyuma imeandikwa jina la Rais Joseph Magufuli tunaomba akamkabizi," alisema.

Advertisement

"Tumemwita Makonda kutokana ni Mwenyekiti wa kamati ya hamasa na jambo hili la kutambulisha jezi ni hamasa basi tumeona vyema kuwaalika na kamati yake na tunatambua mchango mkubwa walioutoa na kamati yake mpaka tunakwenda Afcon," alisema Karia.

Makonda alisema awashukuru wote alioshirikiana katika kamati yake mpaka kufanikisha jambo lao la Taifa Stars kwenda Afcon.

"Jezi hizi ni nzuri na zimebeba rangi ya bendera ya Tanzania na naomba isitokee mtu yoyote akaweka mizengwe kwa kuipenga," alisema Makonda.

"Kwakuwa Watanzania hatuna vazi la Taifa naomba tutumie jezi hizi kuwa kama vazi la taifa katika kipindi hiki cha mashindano na hata pale yatakapomalizika.

"Katika kuhakikisha zinanunuliwa kwa wingi na watu wanavaa tunanunua jezi 100, kwenda kuwapa wajumbe wote wa kamati yangu ya hamsa ili kuonesha nimelipa fadhira na kutambua mchango wangu kwao," alisema Makonda.

UKIWA NA JEZI HAUKAMATWI

Makonda alisema kama akisikia au ikitokea kuna mtu amekamatwa huku akiwa amevaa jezi ya Taifa Stars katika mkoa wa Dar es Salaam ataomba aachiwe huru

"Hii itaonyesha kuwa wewe ni Mtanzania mwenye uzalendo hata kama ukiwa umeiba jezi hii mpya kwa ndani nitaomba polisi wakuache huru pindi nikisikia umekatwa na nikauliza umevaa nini nikaambiwa ni hizi jezi mpya,"alisema.

"Niwakumbushe wale wote ambao watatumia fulsa hii kutengeneza jezi bandia hatuta muacha na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake," alisema Makonda.

Advertisement