TFF yapiga marufuku jezi bandia ya Stars

Muktasari:

TFF imesisitiza kwamba inawaonya wote wanaouza jezi zisizosahihi kuacha mara moja kabla shirikisho hilo halijachukua hatua.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeikana jezi ambayo picha yake imesambaa mtandaoni ikieleza kuwa haihusiki na jezi hiyo.

Taarifa iliyotolewa  Ofisa Habari  wa TFF, Cliford Ndimbo leo Jumapili, imesema kwamba shirikisho hilo limelazimika kutolea ufafanuzi wa jezi za timu ya Taifa zinazozunguka mitandaoni  yenye mtindo wa msalaba kutokana na kuzua mjadala.

TFF imesisitiza kwamba inawaonya wote wanaouza jezi zisizo sahihi kuacha mara moja kabla shirikisho hilo halijachukua hatua.

Aidha, ’Afcon ni Zamu Yetu’, ndivyo wachezaji wa Taifa Stars watakavyoingia uwanjani wakiwa na neno hilo kichwani mwao pale watakapoikabili Uganda katika mchezo wa mwisho wa Kundi L kutafuta nafasi ya kufuzu Fainali za Afrika (Afcon) mwaka huu.

Hakuna kingine zaidi ya Taifa Stars kushinda mchezo huo lakini pia kukazia maombi yote kwa   Cape Verde iifunge Lesotho au itoke nayo sare tu ili Tanzania iandike historia nyingine ya kucheza Afcon kwa mara ya pili tangu ilipofanya hivyo mwaka 1980.

Licha ya Uganda kuwa tayari imeshafuzu Fainali hizo lakini ni wazi haitakuwa tayari kufungwa kirahisi huku kipa wake Dennis Onyango akitaka kuendeleza rekodi yake ya kutoruhusu bao lolote tangu kuanza kwa mashindao hayo hadi fainali.

Ushindi au sare na ushindi wa Cape Verde vitafungua njia ya Tanzania kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 iliyopita.