TFF yapangua hoja za Yanga, yamtosa Manji

Muktasari:

Uchaguzi mkuu wa Yanga utafanyika Januari 13 huku Yanga ikitaka kufanya Uchaguzi kwa nafasi zote kasoro nafasi ya mwenyekiti, wakidai bado wanamtambua Yusuph Manji.

Dar es Salaam. Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imepangua hoja tatu za Kamati ya Utendaji ya Yanga ikiwamo ile ya kutofanya uchaguzi nafasi ya mwenyekiti wa klabu hiyo.

Kamati ya Utendaji ya Yanga iliomba kukutana na kamati ya uchaguzi ya TFF ili kujadili mambo mbalimbali yanayohusu uchaguzi wa klabu hiyo.

Yanga ilikuja na hoja za kutaka wafanye uchaguzi katika nafasi zote kasoro ya mwenyekiti, pia walitaka Kamati ya Uchaguzi ya TFF iwaachie Yanga wasimamie mchakato wa uchaguzi wenyewe na mwisho walitaka wafanye mkutano mkuu kabla ya uchaguzi huku mwenyekiti wao Yusuph Manji akihudhuria.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga waliohudhuria kikao cha leo ni Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Thobias Lingalangala na Siza Lyimo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Malangwe Mchungahela alisema baada ya kikao hicho na Kamati ya Utendaji ya Yanga wameamua kuwa uchaguzi utafanyika kwa nafasi zote kwani hawamtambui Manji kama mwenyekiti wa Yanga kwa sababu alishajiuzuru nafasi hiyo.

"Tulikutana na Kamati ya Utendaji ya Yanga ambayo iliwakilishwa na wajumbe wanne na kuja na hoja zao tatu.

"Hiyo hoja ya kwamba uchaguzi ufanyike kwa nafasi zote kasoro nafasi ya mwenyekiti eti kwa sababu Manji bado ni mwenyekiti Yanga tumeipinga kwa sababu tunachojua Manji alishajiuzuru tangu Mei 20 mwaka jana hivyo ni mwaka sasa umeshapita.

"Katiba ya Yanga inasema mwenyekiti au mjumbe ataachia nafasi yake kwa kujiuzuru kwa barua kwa kuugua, zaidi ya miezi 12 kushindwa kutekeleza majukumu yake au kutohudhuria vikao vinne vya Kamati ya utendaji.

"Juni 10 Yanga ilifanya mkutano mkuu pale Police officers mess Osterbay na licha ya kuwa na ajenda nyingi za kujadili, lakini hazikujadiliwa na hoja ikawa kumrudisha Manji.

"Juni 12 mwaka huu Yanga ilimuandikia barua Manji kumueleza uamuzi wa mkutano mkuu hakujibu. Agosti 9 mwaka huu TFF ilimuandikia barua Manji ili kutaka kujua ni mwenyekiti au sio mwenyekiti sababu walikuwa na barua mbili alijiuzuru mara karudi na walimpa siku saba ajibu, lakini hakujibu.

"Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe alimtafuta ili kujua msimamo wake akamjibu yeye hayupo tayari.

"Sasa kwa uungwana wote huo uliofanyika, lakini yeye hakuwa muungwana na baada ya kusikia Kamati imetangaza uchaguzi ndio tumesikia kamuandikia barua mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Yanga kuwa anarudi.

"Baada ya hapo Oktoba 9 ndipo akajibu na barua ya TFF ambayo sisi kamati ya Uchaguzi, tumeipata Novemba 12"alisema Mchungahela.

"Hoja nyingine walitaka Kamati ya Uchaguzi ya Yanga isimamie mchakato wa uchaguzi yenyewe, lakini tumewakatalia kwa sababu tangu awali walipewa nafasi ya kufanya hivyo mara mbili, lakini hawakutekeleza, hivyo mchakato wa uchaguzi utaendelea kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF Kama kawaida.

"Pia walitaka wafanye kwanza mkutano mkuu Desemba Mosi ambao walisema mwenyekiti wao Manji atahudhuria na tumewaambia hilo halituhusu ila hatumtambui Manji kama mwenyekiti wa Yanga.

"Kama Manji anataka nafasi hiyo aje achukue fomu na kama wanachama wanampenda watampigia kura na kumchagua," alisema Mchungahela.