TFF yamtibulia Kakolanya

Muktasari:

  • Mwanasheria wa TFF, Herman Kidifu alithibitisha kumekuwa na changamoto ndogondogo zinazotokea kiasi cha kufanya kamati hiyo ishindwe kukaa kwa wakati.

KUSUASUA kusikilizwa kwa kesi ya kipa wa Yanga, Beno Kakolanya imeelezwa kunambania kipa huyo kusaka maisha mapya kwingine kwani hakuna dalili za Yanga kumfungulia tena milango aidakie.

Kesi hiyo iliwasilishwa kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ili kutoa hatma ya Kakolanya dhidi ya Yanga, lakini imekuwa ikipigwa danadana kutokana na sababu mbalimbali.

Ukimya wa kamati hiyo kuamua hatma yakipa huyo, imemfanya Kakolanya kukaa mtaani tu, licha ya maisha yake kutegemea soka, pia ukimya huo umemfanya ashindwe kusaini timu nyingine mpya.

Awali Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Elias Mwanjala alikaririwa na Mwanaspoti akisema wangekutana kabla ya Aprili 12 lakini kumekuwa na ukimya bila majibu yoyote baada ya tarehe hiyo kupita.

Mwanasheria wa TFF, Herman Kidifu alithibitisha kumekuwa na changamoto ndogondogo zinazotokea kiasi cha kufanya kamati hiyo ishindwe kukaa kwa wakati.

“Ila kwa sasa siku yoyote kuanzia Jumanne kamati inaweza kukaa. Hizi kamati zinaitishwa na Mwenyekiti au Katibu Mkuu, ofisi yangu inakuwa inaandaa tu,” alisema Kidifu.

Msemaji wa TFF, Clifford Ndimbo alitafutwa ili kujua ukimya huo baada ya Kidifu kutaka atafutwe ili afafanue naye, alisema Kamati hiyo ikikaa basi umma utaambiwa na majibu yatakayopatikana.

“Kumekuwa na utaratibu wa kila taarifa kuwekwa wazi vikao vinapofanyika, hivyo hata wakikaa basi taarifa zitakuwa wazi kama utaratibu ulivyo,” alisema kwa kifupi.