TFF yamtetea refa aliyeboronga Yanga dhidi ya Kagera Sugar

Muktasari:

Waamuzi wamekuwa wakilalamikiwa mara kwa mara katika maamuzi yao ambayo yanazigharimu timu nyingine ndani ya dakika 90


KAMATI ya Waamuzi hapa Nchini imemkingia kifua Mwamuzi wa mchezo wa jana kati ya Yanga na Kagera Sugar Shomari Lawi kutokana na sintofahamu juu ya maamuzi yake katika penati iliyowapa Yanga ushindi.

Jana Yanga ilikuwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini kukabiliana  na Kagera Sugar katika mchezo wa kombe la FA ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 na kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayotoa mwakilishi wa kombe la Shirikisho  Afrika mwakani.

Akizungumza na Mwanaspoti Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Israel Nkongo ambaye ni mwamuzi mstaafu kwa sasa alisema, hawezi kumuhukumu mwamuzi Lawi kutokana na makosa ya kibidamu yaliyotokea katika mchezo wa jana.

Amesema mwamuzi akiwa katika majukumu yake anafanya maamuzi kulingana na jinsi ambavyo aliona tukio kwa wakati huo. 

"Mechi ya jana maamuzi yake ndicho alichokiona ila nyie kwa kuwa mmeangalia mara kwa mara katika runinga ndio mmeona hayo makosa baada ya kuangalia kwa kurudia rudia.

"Yeye pia ni binadamu pale ndani ya uwanja hana sehemu ya kuangalia mara mbili kama nyie mnaoangalia katika runinga na kuanza kumlalamikia, najua hata yeye hapo baadae akija akakaa na kuangalia kama nyie anagundua kulikuwa na shida," alisema Nkongo.

Aidha Nkongo amesema hata yeye wakati alipokuwa anachezesha akimaliza mechi na kwenda kuitizama marudio alikuwa akibaini mapungufu juu yake na kuyafanyia kazi zaidi ili yasijirudie.

Amesema Lawi anatakiwa kutumia sintofahamu hiyo ili yasijirudie tena makosa hayo katika mechi nyingine ambazo atachezesha.

Nkongo amesema kwa kuona hayo mapungufu katika mchezo wa Simba na Azam watachezesha waamuzi sita ili punguza makosa ya kibinadamu na kukiri kutamani kiwatumia waamuzi hao katika kila mechi ila ufinyu wa bajeti unawakwamisha.

Lawi amekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii toka jana baada ya Mrisho Ngasa kuchezewa madhambi nje ya boksi na kuangukia ndani huku mwamuzi huyo akiamuru ipigwe penati ambayo imewapa Yanga nafasi ya kutinga nusu fainali.