TFF yalia makatibu wakuu klabu kuingia mitini

Muktasari:

  • Semina hiyo ina lengo la kuwajengea uelewa makatibu kuhusu mashindano ya timu zao za vijana na masuala ya uendeshaji wa klabu kwa kila siku

Dar es Salaam. Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimesikitishwa na kitendo cha klabu nyingi kutuma wawakilishi katika semina ya Makatibu wakuu wa klabu za Ligi Kuu inayofanyika leo jijini Dar es Salaam.

Katika semina hiyo inayofanyika kwenye Hotel ya Demage Kinondoni, Makatibu wakuu wengi wa klabu hawakuhudhuria huku wengine wakituma wawakilishi.

Wakati wa ufunguzi wa semina hiyo Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alishangazwa na klabu kuleta watu wengine ambao sio walengwa wa semina hiyo.

"Inashangaza kuona klabu zimeleta watu wengine ambao hawafanyi kazi za kila siku za klabu kwa sababu nia na madhumuni yetu ni kuwajengea uwezo makatibu wakuu kutambua wajibu wao na kutimiza kwa ufasaha kazi zao katika klabu kwa maendeleo ya mpira miguu"alisema Kidao.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto amesikitishwa na makatibu wachache kuhudhuria semina hiyo na kusema hii sio mara ya kwanza viongozi kudharau semina mbalimbali zinazoandaliwa kwa ajili yao.

"Inasikitisha kuona mahudhurio ni hafifu na klabu nyingi zimetuma wawakilishi na hii inatokana na wengi hawafahamu umuhimu wao kama makatibu na nguvu yao katika klabu.

"Hii sio mara moja wanafanya hivyo na hatujui nia na dhamira yao ya kuendeleza mpira," alisema Mguto.

Aliongeza "Wanaweza kujitetea ni ukata umewakwamisha, lakini hapana kwani kila kitu wanagharamiwa.

Alisema semina hiyo pia ilikuwa na lengo la kuwajengea uelewa makatibu kuhusu mashindano ya timu zao za vijana ambazo kila klabu inatakiwa kuwa na timu hizo kwa mujibu wa kanuni za Ligi.