TFF kuua ndege wawili

Muktasari:

  • Katika mkutano huo utakaoenda sambamba na uchaguzi huo mdogo, Arusha itakosa uwakilishi wa kutosha kutokana na kufungiwa kwa viongozi wanne wa Chama cha Soka Mkoa (ARFA) kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mapato ya mechi ya kirafiki ya Arusha United na Simba.

ARUSHA .UKISIKIA kuua ndege wawili kwa jiwe moja ndiko huku, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limepanga kufanya mikutano miwili ya mwaka kwa wakati mmoja, ule wa mwaka huu na wa 2018 uliokwama kufanyika kwa sababu mbalimbali.

Kwa mujibu wa Afisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo shirikisho hilo litafanya mkutano wa kwanza wa 2018 Februari 3, jijini hapa. Awali mkutano huo ulipangwa kufanyika Feb 2, lakini Ndimbo alisisitiza utafanyika Feb 3.

“Mkutano wa Febuari 3 ni mkuu wa mwaka 2018 ulioshindwa kufanyika kwa sababu ya kalenda ya uchaguzi mdogo, kisha mwishoni mwa mwaka huu tutafanya mkutano mwingine kwa mwaka 2019,” alisema.

Uchaguzi mdogo wa TFF ni wa kuziba nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Uwakilishi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara na ule wa Simiyu na Shinyanga.

Katika mkutano huo utakaoenda sambamba na uchaguzi huo mdogo, Arusha itakosa uwakilishi wa kutosha kutokana na kufungiwa kwa viongozi wanne wa Chama cha Soka Mkoa (ARFA) kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za mapato ya mechi ya kirafiki ya Arusha United na Simba.

Mkoa huo utawakilishwa na kiongozi mmoja pekee, Katibu wa ARFA Zakayo Mjema, huku ikiwakosa wawakili watatu wakiwamo Mwakilishi wa Klabu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu) ambazo hazikuwa na viongozi kimkoa katika uchaguzi uliopita.